IAEA Iran
9 Novemba 2011Katika muktadha huo huo, kwa mara ya kwanza ripoti hiyo inaonesha kuwa na wingi wa uelewa wa mpango huo, ambao kwa ujumla wake haukujulikana hapo mwanzoni. Inasema kuwa wanasayansi wa Iran wanaendelea kufanya kazi kuthibitisha uwezo wao wa teknolojia ya nyuklia, na hivyo kuongeza matumizi yake kwa madhumuni ya njia za amani kama ilivyo kwa njia za kijeshi.
Lakini hata Ujerumani nayo inao utaalamu huo wa kutengeneza silaha za nyuklia, ingawa imejitangaza zamani kutokujihusisha na silaha hizo. Tafauti ni kuwa, hadi sasa Iran haijafanya hivyo. Utawala wa viongozi wa kidini wa nchi hiyo, umewacha milango wazi katika hilo, na badala yake wanafanya kazi kifichoficho na kwa msaada wa wanasayansi kutoka nje, kama tunavyojua sasa, kuimarisha matumizi ya kijeshi ya teknolojia hiyo, kama vile kuweka vichwa vya nyuklia kwenye makombora au vifaa vya miripuko.
Baina ya uelewa huu mpya, kuna mambo mengine mengi pia ya kuyazingatia. Kwanza pana tafauti kati ya kuwa na uwezo wa kutengeneza silaha na kuzitengeneza. Na pili pana tafauti baina ya kuwa na silaha hizo na uamuzi wa kuzitumia. Hapo ndipo penye kitisho cha wazi dhidi ya amani ya Isreal na kwa amani ya dunia, bali pia hata kwa Ulaya. Sasa nini cha kukifanya?
Kwa kutumia njia za kidiplomasia, imejaribiwa kwa mwaka mzima kuitaka Iran iachane na silaha za nyuklia. Katika muongo uliopita, kwa kushirikiana na Wakala wa Atomiki wa Ujerumani, kuna hatua kadhaa zimepigwa katika njia hii. Lakini kwa Israel, wanaona kwamba sasa hakuna linaloweza kufanywa tena kidiplomasia.
Lakini mashambulizi ya kijeshi dhidi ya mpango wa nykulia wa Iran si chaguo hata kidogo. Hayatolimaliza suala la nyuklia la Iran na pengine hata hayataliharibu, labda tu kuchochea mgogoro wa kisiasa. Yataimarisha mahusiano baina ya raia wa Iran na utawala wao, hasa ikizingatiwa kuwa nchi hiyo imefungwa kutoka athari za ulimwengu wa nje, hasa mataifa ya magharibi. Chuki dhidi ya mataifa hayo zitazidi. Hilo si jambo ambalo Israel ingelitaka litokezee, na hivyo itamlazimu Mshindi wa Nishani ya Amani ya Nobel, Barack Obama, ajiepushe nao.
Uwezo wa kushambulia wa Israel unafahamika sana na Iran. Imetishia mara kadhaa kuishambulia nchi hiyo, hata ikiwa itachukuwa hatua hiyo peke yake, kwa kile inachosema ni kujilinda.
Lakini ripoti ya Shirika la Nguvu za Atomiki la Umoja wa Mataifa sasa iko mikononi mwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Huko kutaamuliwa vikwazo zaidi dhidi ya Iran. Huko nako lazima sasa Urusi isiwe tena kikwazo, kwa kusimamisha hatua kali dhidi ya Iran. Maana ukweli mchungu ni kwamba ni pale tu vikwazo vya kimataifa dhidi ya Iran vinapoimarishwa, ndipo nchi hiyo inapokuja kwenye meza ya mazungumzo.
Vivyo hivyo, lazima sasa ifikiriwe njia nyengine nje ya vikwazo na nje ya mashambulizi ya kijeshi. Tayari vikwazo vya kiuchumi na kutengwa kwa uongozi wake kumeshaiweka pabaya nchi hiyo. Lakini nguvu ya viongozi wa kidini kwa umma wa Iran haijapunguzwa, kama ambavyo walioko nje wangelipenda kuona. Ikiwa jumuiya ya kimataifa itatoa fursa ya kufanya kazi kiuchumi na pia matumizi ya amani ya nishani, uwiano wa nguvu za utawala unaweza kubadilishwa na hatimaye kulainisha kabisa msimamo mkali wa utawala huo. Dhamira hatimaye ni kuizuia Iran kuwa taifa linalomiliki bomu la nyuklia.
Mwandishi: Daniel Scheschkewitz
Tafsiri: Mohammed Khelef
Mhariri: Othman Miraji