Mashambulizi ya anga yauwa 40 Yemen
27 Machi 2015Maafisa wa wizara ya afya inayodhibitiwa na waasi wa Kihouthi imesema watu 12 ni miongoni mwa wahanga waliouwawa wakati shambulio la anga kaskazini mwa Sanaa kupiga kwenye maeneo ya makaazi ya watu.
Mashahidi wamesema ndege za kivita zililenga mashambulizi yake dhidi ya kambi ya Al-Samaa ambayo inatumiwa na vikosi vya kijeshi ambapo inaaminika kuwa hupokea amri kutoka kwa kamanda wa zamani Ahmed Ali Saleh ambaye ni mtoto wa Rais aliyeondolewa madarakani Ali Abdullah Saleh anayetuhumiwa kushirikiana na waasi wa Kihouthi dhidi ya Rais Abderabbo Mansour Hadi.
Kufikia aljajiri ya leo mashambulizi matatu ya anga yamepiga makaazi ya rais kusini mwa Sanaa ambayo waasi waliyateka mwezi uliopita.Wakati wa usiku pia kulifanyika mashambulizi dhidi ya kikosi cha kijeshi kilicho tiifu kwa Saleh katika jimbo la mashariki la Marib.
Operesheni za mafanikio
Afisa wa kijeshi ameliambia shirika la habari la AFP kwamba ndege za kivita za nchi washirika zikiongozwa na Saudi Arabia pia zilishambulia kwa mabomu bohari kubwa ya silaha katika kambi ya tatu ya kijeshi inayotumiwa na vikosi vilivyo tiifu kwa rais wa zamani aliyekuwa na ushawishi mkubwa nchini humo.
Mshauri wa waziri wa ulinzi wa Saudi Arabia Ahmad Bin Hassan Asiri amesema mashambilizi hayo yamekuwa na mafanikio.Amesema"Ni operesheni ya mafanikio ambapo ndege nyingi za kivita zimeshiriki.Saudia inaoongoza operesheni hiyo tumefanikisha malengo yetu dakika 15 za kwanza za operesheni hiyo na tumeendelea hadi tulipokamilisha malengo yote tuliyojiwekea."
Maelfu ya waandamanajji wameandamana hapo Alhamisi katika mji mkuu wa Sanaa kuwaunga mkono Wahouthi kufuatia mashambulizi hayo yaliyoongozwa na Saudi Arabia.
Wayemen hawatosalimu amri
Kiongozi wa kundi la wasi la Wahouthi Abdul Malik al Houthi amezishutumu Marekani,Saudi Arabia na Israel kwa kuanzisha mashambulizi yenye nia ya kuivamia na kuikalia kwa mabavu Yemen.
Houthi amekaririwa akisema "Wananchi wetu vipenzi wa Yemen ni watu walioko huru na katu hawatoingizwa utumwani na mtu yoyote yule.Iwapo utawala wa kipumbavu na dhuluma wa Saudi Arabia unadhani wananchi wa Yemen watawasujudia na kusalimu amri kwao tunasema hapana,mara elfu hapana hilo katu halitotokea."
Pakistan bado haikutowa uamuzi iwapo itowe msaada wa kijeshi kwa Saudi Arabia katika mashambulizi hayo inayoyaongoza dhidi ya wasi wa Kihouthi nchini Yemen lakini imeahidi kuilinda Saudi Arabia dhidi ya tishio lilote lile kwa mshikamano wao.
Waziri wa ulinzi wa Pakistan Khawaja Asif ameliambia bunge hapo Ijumaa kwamba hawakuamua kushiriki katika vita hivyo na hawakutowa ahadi yoyote ile ya kutowa msaada wa kijeshi kwa ushirika huo unaongozwa na Saudi Arabia kupambana na waasi wa Kishia nchini Yemen.
Rais wa Yemen Abd Rabu Mansour Hadi amewasili Saudi Arabia kutoka Aden ambako alikuwa amejihifadhi baada ya kukimbia kifungo cha nyumbani katika mji mkuu wa Sanaa.
Mwandishi : Mohamed Dahman/Reuters/AFP
Mhariri:Yusuf Saumu