Mashambulizi pacha yauwa zaidi ya 20 Msikitini Nigeria
1 Mei 2018Msemaji wa polisi katika jimbo la Adamawa, Othman Abubakar, amesema mripuko ulitokea wakati wa swala ya adhuhuri siku ya Jumanne, na watu wengi walikufa wakati wakikimbia na kukutwa na mripuko mwingine. Abubakar amesema eneo la tukio katika mji wa Mubi limezingirwa na vikosi vya kupambana na mabomu pamoja na maafisa wa usalama.
Wakaazi wa eneo hilo wanasema mwanaume kijana alievalia vesti ya kujiripua aliingia msikitini pamoja na waumini wengine. Mkaazi mmoja alisema paa la msikiti huo liliezuliwa. Wengi wanalilaumu kundi la Boko Haram kwa kuhusika na shambulio hilo.
Duru kutoka hospitali kuu ya Mubi zimesema "mpaka sasa tumepokea maiti 37 na dazen kadhaa za majeruhi kutoka kwenye maeneo mawili ilikotokea miripuko."
Hakukuwa na taarifa rasmi juu ya idadi ya vifo. Chanzo cha hospitali, kilichoomba kusalia kapuni kwa sababu hakiruhusiwi kuzungumza na vyombo vya habari, kiliongeza kuwa: " Idadi ya vifo inaweza kuongezeka kwa sababu uhamishaji bado haujakamilika. "Wengi wa waliojeruhiwa walikuwa katika hali mbaya na huenda wasipone."
Wafanyakazi kutoka hospitali hiyo walihamasishwa kuwashughulikia waathirika, licha ya kuwa kwenye mgomo kudai malipo zaidi na kuboreshwa kwa mazingira ya kazi.
Mubi hushambuliwa mara kwa mara
Mkaazi wa Mubi Abdullahi Labaran alisema mripuaji wa kwanza alijichanganya na waumini waliokusanyika kwa ajili ya swala katika msikiti ulioko karibu na soko. Mubi iko umbali wa kilomita 200 kutoka Yola.
Umelengwa mara kwa mara na mashambulizi mabaya yanayolaumiwa kwa kundi la Boko Haram tangu ulipotekwa kwa muda mfupi na wanamgambo hao mwishoni mwa mwaka 2014.
Novemba 21, 2017 watu wasiopungua 50 waliuawa wakati mripuaji wa kujitoamuhanga alipojiripua katika msikiti wakati wa swala ya Alfajiri katika eneo la Unguwar Shuwa mjini Mubi.
Oktoba 2012, watu wasiopungua 40 waliuawa katika shambulio dhidi ya nyumba ya wanafunzi mjini Mubi ambalo lililaumiwa kwa sehemu kubwa kwa Boko Haram. Juni 2014, mashabiki wasiopungua 40 wa kandanda, wakiwemo watoto na wanawake, walikufa katika shambulio la bomu baada ya mechi katika eneo la Kabang mjini humo.
Mwandishi: Iddi Ssessanga/afpe, ape
Mhariri: Mohammed Khelef