1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mashambulizi nchini Syria yaendelea kuwaua raia

6 Februari 2018

Watu 29 wameuawa katika mashambulizi ya anga Syria kwenye eneo linalodhibitiwa na waasi karibu na Damascus. Mauaji hayo yamefanyika wakati vita vya maneno kuhusu matumizi ya gesi ya chlorine dhidi ya raia yakiendelea.

https://p.dw.com/p/2sB15
Angriffe des Assad-Regimes in Goutha, Syrien
Picha: picture alliance/abaca/A. Al Bushy

Mauaji hayo yametokea jana baada ya mashambulizi kadhaa ya anga na ufyatuaji wa makombora katika eneo la Ghouta Mashariki, wakati ambapo mzozo wa Syria uliodumu kwa miaka saba ukiwaacha raia wakiteseka. Mkurugenzi wa shirika linalofuatilia haki za binaadamu nchini Syria, Rami Abdel Rahman amesema raia 29 waliuawa na wengine kadhaa walijeruhiwa. Mashambulizi hayo yametokea katika soko kwenye mji wa Beit Sawa na kuwaua raia 10 wakiwemo watoto wawili.

Raia wengine tisa wakiwemo watoto wawili na mfanyakazi mmoja wa shirika la uokozi waliuawa katika eneo la Arbin. Wakaazi wa maeneo kadhaa ya mapambano nchini Syria wameripoti kuongezeka kwa mashambulizi na wameyashutumu majeshi ya serikali ya Syria kwa kutumia silaha za sumu dhidi ya maeneo yanayodhibitiwa na waasi.

Syrien Idlib Giftgasangriff
Watoto wakitibiwa Syria baada ya kuathiriwa kwa sumu ya chlorinePicha: picture-alliance/abaca/S. Zaidan

Jana Marekani ilisema kuna ''ushahidi wa wazi'' kwamba palikuwa na mashambulizi kadhaa ya silaha za sumu katika wiki za hivi karibuni, yakiwemo kwenye maeneo ya waasi Ghouta Mashariki. Marekani na Urusi zilizozana jana katika kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kutokana na Marekani kushinikiza iandaliwe taarifa ya kulaani madai kwamba mashambulizi ya silaha za sumu yalitumika nchini Syria na kusababisha watu wengi kujeruhiwa, wakiwemo watoto.

Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa, Nikki Haley ameikosoa Urusi kwa kumlinda Rais wa Syria Bashar al-Assad kutowajibishwa kwa kile alichokifanya.

Kinachoendelea Syria kinaiogopesha dunia

''Waathirika wa kile kinachoonekana kuwa sumu ya chlorine wanamiminika hospitalini. Matukio machache yameigopesha nchi yangu na dunia nzima kwa ujumla, ikiwa utawala wa Assad utatumia silaha za sumu dhidi ya watu wake. Baraza hili limekuwa likiikemea na kuitaka Syria kuacha kutumia silaha za sumu, lakini bado inaendelea,'' alisema Haley.

Marekani inapendekeza itolewe taarifa kulaani matumizi ya sumu kama silaha, lakini Urusi ambayo ni mshirika wa serikali ya Syria ikaongeza marekebisho katika taarifa hiyo ambayo haikugusia chochote kuhusu mashambulizi hayo na mwisho wa siku hakuna taarifa yoyote iliyotolewa.

USA New York Abstimmung Chemiewaffenuntersuchung in Syrien
Balozi wa Marekani UN, Nikki HaleyPicha: Reuters/B. McDermid

Balozi wa Urusi katika Umoja wa Mataifa, Vassily Nebenzia amesema ni wazi lengo lilikuwa kuishutumu serikali ya Syria kwa matumizi ya silaha za sumu, wakati ambapo hakuna mhalifu ambaye ametambuliwa.

Wakati huo huo, Syria imepeleka vikosi vya ulinzi na mfumo wa kijikinga na makombora kwenye maeneo ya mapambano katika majimbo ya Aleppo na Idlib.

Ama kwa upande mwingine, mwanajeshi mmoja wa Uturuki ameuawa katika shambulizi la roketi lililofanywa na wanamgambo wakati vikosi vya Uturuki vikiweka kambi ya kijeshi kaskazini magharibi mwa Syria. Vikosi vya Uturuki vimesema leo kuwa wanajeshi wengine watano wa Uturuki walijeruhiwa.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFP, AP, Reuters
Mhariri: Josephat Charo