Mashambulizi Iraq.
10 Agosti 2009Watu 33 wameuawa huko Kaskazini mwa Iraq, katika eneo la wafuasi wa dhehebu la wasunni, kufuatia mripuko mkubwa wa bomu. Shambulizi hilo ni mfulilizo wa mashambulizi yanayofanyika nchini Iraq tangu vikosi vya Marekani kuondoka katika miji ya Iraq, mwezi uliopita.
Mfulilizo wa mashambulizi nchini Iraq..yanazidi kuibua wasiwasi iwapo vikosi vya Iraq viko tayari kudhibiti usalama wa nchi hiyo, kutoka kwa vikosi vya Marekani vinayvojitayarisha kuondoka kabisa nchini Iraq- miaka minane baada ya kuivamia nchi hiyo kumng'oa madarakani rais Saddam Hussein.
Miripuko hii ya bomu pia inatia wasiwasi ya kuzuka tena kwa mauaji ya kikabila kati ya Wasunni na Washia. Umwagikaji wa damu ulikuwa kidogo umepungua katika miezi kumi na nane iliyopita, lakini kabla ya hapo.....kila siku maiti zilihanikiza barabara za Iraq, pale makundi ya Washia na Wasunni waliposhindana kumalizana.
Mashambulizi ya leo, ya bomu yalipishana tu kwa dakika 15, lori lililokuwa na bomu liliripuka alfajiri katika kijiji cha Khazna huko Mosul na watu 26 wakauawa huku wengine 128 wakijeruhiwa. Mripuko huo uliporomosha kiasi cha nyumba 40, na watu kadhaa wanasemekana walizikwa chini ya mabaki ya nyumba hizo.
Visa vya miripuko ya bomu na ufyatulianaji risasi huripotiwa kila siku huko mosul- eneo ambalo limekabiliwa na cheche kali za uhasama kati ya jamii ya Waarabu na wakurdi na kutishia kuwaangamiza wakaazi na kuutingisa kabisa uzi unaoshikilia usalama nchini Iraq.
Kutokana na hali yake tete, wapiganaji wenye itikadi kali wamepata makaazi Mosul na wanachangia zaidi mzozo katika eneo hilo.
Wiki iliyopita, watu 44 waliuawa kufuatia mfulilizo wa miripuko ya mabomu yaliyowalenga jamii ya Washia katika mji mkuu wa Baghadad pamoja na Kaskazini mwa Iraq.Kundi la Al-Qaeda lililaumiwa kwa kuhusika na shambulio hilo.
Mjini Baghdad bomu lililokuwa limetegwa ndani ya gari liliwaua watu saba waliokuwa wamepanga foleni kusubiri kuajiriwa kibarua, nje ya kampuni moja, mjini humo.
Ingawa umwagikaji wa damu umepungua kidogo katika miezi 18 iliyopita-bado wapiganaji wenye itikadi kali wanaendelea kuwakabili maafisa wa usalama wa Iraq ambao bado wanajaribu kujifunza jinsi ya kukabiliana na mashambulizi nchini humo. Mwezi wa Julai idadi ya watu waliouawa nchini iraq ilipungua kutoka 374 hadi 224 .
Vikosi vya Marekani vimepangiwa kuondoka kabisa nchini Iraq mwaka 2012- kuambatana na makubaliano kati ya Marekani na Iraq. Waziri wa ulinzi wa Marekani Robert Gates alidokeza kwamba Marekani huenda wakaondoka kwa haraka nchini Iraq iwapo vikosi vya usalama nchini humo vitaimarisha hali ya usalama. Uchaguzi Januari mwakani utakuwa changamoto kubwa na mtihani mkubwa Iraq kudhidhirisha kwamba wako tayari kushikilia usalama wa nchi yao mikononi mwao.
Mwandishi: Munira Muhammad/ RTRE
Mhariri: Abdul-Rahman.