Mashambulizi dhidi ya Wahouthi yaendelea
30 Machi 2015Mkaazi mmoja wa Sanaa amesema inaonekana mashambulizi hayo kwa kiasi kikubwa yamelenga maeneo yalio karibu na Kasri la Rais yanayopakana na eneo la makaazi ya ofisi za kibalozi mjini humo.
Mwanadiplomasia mmoja wa Yemen amekaririwa akisema "ulikuwa ni usiku wa jahanam."
Wakaazi wanasema mashambulizi hayo pia yamelenga bohari za silaha karibu na mlima Nugum ambao unaangaliana na mji huo.Wizara ya afya inayodhibitiwa na vuguvugu la Wahouthi imesema hapo jana mashambulizi hayo yameuwa watu 35 na kujeruhi wengine 88 usiku wa Jumamosi kuamkia Jumapili.Idadi hiyo haikuweza kuyakinishwa na duru zilizo huru.
Wahouthi wanyemelea Aden
Mji wa Aden unaoshikiliwa na wafuasi wa Rais Hadi milio ya risasi za bunduki za rashasha na miripuko ya mabomu imekuwa ikisikika hadi usiku wa manane hapo jana katika mji huo mzima wa bandari ulioko kusini mwa Yemen.
Hakuna habari zilizoweza kupatikana mara moja juu ya chanzo cha mapambano hayo ya Aden lakini inaelezwa zilikuwa ni harakati mpya za waasi wa Kishia wa jamii ya Wahouthi na washirika wao wapiganaji walio tiifu kwa rais wa zamani wa nchi hiyo Ali Abdulllah Saleh kusonga mbele kuingia katika kitongoji cha Sheikh Uthman mjini Aden. Hakuna taarifa juu ya maafa.
Mkutano wa Umoja wa Kiarabu wa siku mbili uliomalizika Jumapili Sharm el Sheikh nchini Misri ulihodhiwa na suala la mzozo huo wa Yemen.
Nchi wanachama wa Umoja wa Kiarabu zimetowa wito kwa waasi wa Kihouthi kuondoka mara moja katika mji mkuu wa Sanaa na kuunga mkono kikamilifu operesheni hizo za kijeshi zinazoongozwa na Saudi Arabia ambayo imesema hazitosita hadi hapo waasi hao watakaposalimu amri na kusalimisha silaha zao.
Wahouthi wataka kuanzisha taifa la Kishia
Serikali ya Yemen inawashutumu waasi hao kwa kujaribu kuipinduwa serikali na kuanzisha taifa la Washia.Iran nchi ya Kishia ambayo inakanusha kuwasaidia wanamgambo hao wa Kihouthi imelaani mashambulizi hayo.
Baadhi ya vituo vya televisheni vya nchi za Kiarabu vimesema wapiganaji wa Kihouthi wako kama kilomita 30 kaskazini nwa Aden.
Gazeti la Aden al -Ghad limechapisha picha za vifaru kadhaa, magari ya deraya na magari mengine ya kijeshi yalioteketea ambayo inasema yameteketezwa wakati wa mapigano ya hivi karibuni.
Mwandishi: Mohamed Dahman/Reuters
Mhariri: Mohammed Khelef