1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mashambulio ya kujitoa muhanga yaitikisa Iraq

Saumu Mwasimba28 Julai 2008

Miji ya Baghdad na Kirkuk yashuhudia wimbi hilo kubwa la mashambulio yaliyofanywa na washambuliaji wa kike

https://p.dw.com/p/ElOy
Maafisa wa usalama wa Iraq wakilinda barabara wakati mahujaji wakielekea msikiti mtakatifu mjini Baghdad.Picha: AP

Polisi nchini Iraq imetangaza hali ya kutotoka nje kwenye mji wa kaskazini wa Kirkuk hadi kesho alfajiri kufuatia shambulio la bomu la kujitoa muhanga ambapo watu 22 waliuwawa na wengine 150 wakajeruhiwa.

Hii leo washambuliaji wanne wa kujitoa muhanga wanaosadikiwa kuwa wanawake wamejiripua na kuua takriban watu 60 na kuwajeruhiwa wengine 165 katika miji ya Baghdad na mji wa kaskazini wa Kirkuk.

Polisi nchini humo imesema mashambulio hayo ndio mabaya kabisa kuwahi kushuhudiwa nchini humo katika kipindi cha miezi kadhaa.

Mjini Baghdad washambuliaji watatu wamejiripua katikati ya umma wa mahujaji wakishia na kuua watu 25 na 40 wakajeruhiwa.

Msemaji wa jeshi la Iraq Qasim Atta amethibitisha kwamba wanawake watatu waliojifunga mikanda ya mabomu walishambulia maeneo matatu katika wilaya ya kati ya karada.

Washambuliaji hao walijivurumisha kwenye msafara wa mahujaji hao wakiekea katika msikiti mtakatifu wa Kadimiya kaskazini magharibi mwa Baghdad kuadhimisha kifo cha Imami wa karne ya nane Imam Musa al Kazim aliyezikwa katika msikiti huo.

Maelfu ya wanajeshi wa Iraq na wa Marekani wamepelekwa katika eneo hilo kufuatia hali ya wasiwasi iliyojitokeza kutokana na mashambulizi hayo.

Kwa mara ya kwanza walinzi wa kike wamepelekwa katika eneo hilo kwa lengo la kuwapekua wanawake wanaohudhuria maadhimisho hayo yatakayofikia kilele chake hapo kesho jumanne.

Katika mji wa Kirkuk kaskazini mwa Iraq mshambuliaji wa kike aliulenga mkusanyiko wa wakurdi waliokuwa wakihudhuria mkutano wa maandamano ya kupinga hatua ya bunge ya kupitisha muswaada wa sheria ya uchaguzi.

Alijiripua na kuua kiasi cha watu 22 na kuwajeruhi wengine 125.

Waandamanaji wenye hasira wakiwa wamebeba mabango yaliyotapakaa damu na fimbo waliyavamia maduka kadhaa wakilaumu kwamba mashambulio hayo yamelengwa kwa jamii ya waarabu wa eneo hilo na jamii ya waturuki.

Waturuki wa Iraq wametoa taarifa wakisema kwamba watu waliokuwa na silaha kutoka jamii ya wakurdi walivamia ofisi zao huku mashahidi wengine wakiripoti kwamba wakurdi hao waliokuwa na silaha walizingira ofisi hizo baada ya shambulio la Bomu.

Hata hivyo hadi sasa hakuna kundi lolote lililodai kuhusika na mashambulio hayo ya mjini Baghdad na Madain lakini makundi ya wasunni wenye siasa kali na hasa Al Qaeda nchini Iraq wamekuwa mara nyingi wakiwalenga mahujaji wakishia wakati wa sherehe kama hizo zinazofanyika kila mwaka.

Wakati hayo yakiarifiwa na hali ikiwa ni tete kwenye eneo hilo Marekani imetoa taarifa ya kulaani wimbi hilo la mashambulio ya kujitoa muhanga na kuwatolea mwito wa Iraq kuwa watulivu.