1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mashambulio ya kigaidi ya Sri Lanka Magazetini

Oumilkheir Hamidou
24 Aprili 2019

Mashambulio ya kigaidi nchini Sri Lanka, rais wa Marekani Donald Trump na suala la wakimbizi na jinsi nchi za magharibi zinavyomyooshea mikono rais mteule wa Ukraine ni miongoni mwa mada magazetini.

https://p.dw.com/p/3HKIu
Sri Lanka Negombo Zerstörte St. Sebastian Kirche nach Anschlag
Picha: Reuters/A. Perawongmetha

Tunaaanzia Sri Lanka ambako magaidi wa itikadi kali wanadai eti mashambulio yao yamelenga kulipiza kisasi cha yale mashambulio ya mwezi uliopita yaliyofanyika misikitini mjini Christchurch nchini New-Zealand. Gazeti la "Badische Zeitung" linazisuta hoja hizo na kuandika: "Hata kama hoja hizo mtu angeweza kusema ni zenye kuingia akilini lakini ukweli ni kwamba zinapotosha. Kwa sababu mtandao wa kimataifa wa kigaidi wa wanajihadi wanaojiita wa Dola la kiislam, waliodai kuhusika na mashamabulio ya jumapili iliyopita, hawahitaji mauwaji ya waislam wapenda amani, ili kuwalenga raia wa mataifa ya magharibi. Magaidi hao wa itikadi kali wanauwa kwa sababu ya chuki, wanapendelea zaidi kuwauwa wakristo kokote kule wanakoweza kufanya hivyo. Lakini  wengi wa wahanga wao ni waislam."

Mkamia maji hayanywi

Wahenga wanasema mkamia maji hayanywi. Methali hiyo ndiyo iliyotumiwa na mhariri wa gazeti la"Mittelbayerische Zeitung" kuzungumzia kisa cha rais wa Marekani Donald Trump na wakimbizi. Gazeti linaandika: "Trump anaonyesha hajui afanye nini. Kwa sababu sheria  hawezi kuzibadilisha kama atakavyo yeye na mahakama mara kadhaa yameshamzuwia. Kwa hivyo mfuasi huyo wa siasa kali za kizalendo hana budi isipokuwa kushuhudia jinsi kila mwezi watu wasiopungua  100,000 wanavyoingia nchini humo kutoka nchi za  Amerika ya kati. Badala ya kushughulikia chanzo cha ukimbizi ,Trump anazidi kuwashinikiza watu wayahame maskani yao. Wakati huo huo anatunisha misuli na kuwarejesha  makwao, wafuasi wa magenge ya makatili. Huko wanafanya yale yale waliyojifunza walipokuwa majiani LA, Houston, au Chicago."

Nchi za magharibi zamnyooshea mkono  rais mpya wa Ukraine

 Mada yetu ya mwisho magazetini inatupeleka Ulaya ya mashariki nchini Ukraine ambako wananchi wenye kiu cha mageuzi wamemchagua mchekeshaji asiyekuwa na maarifa yoyote ya kisiasa  kuwa rais wa nchi hiyo. Licha ya mizozo ya nchi hiyo na Urusi inayowaunga mkono waasi wanaopigania kujitenga jimbo la Donbass na rasi ya Crimea, inayodhibitiwa na Urusi. Gazeti la "Volksstimme" linaandika: "Hata kabla ya Volodymyr Zelenskiy  kutawazwa mshindi wa uchaguzi, ameshaanza kukumbatiwa na nchi za magharibi. Marekani imeahidi kusaidia dhidi ya " uchokozi wa Urusi", serikali kuu ya Ujerumani imeelezea utayarifu wake wa kumuunga mkono katika kulinda mamlaka ya nchi hiyo..Yote hayo yanaweza kuwa ni sawa. Suala linalozuka lakini ni jee kipa umbele ni kipi baada ya uongozi kubadilika mjini Kiev?"

 

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/INlandspresse

Mhariri: Daniel Gakuba