Mashamba, machimbo Pakistan taabani kuondoka kwa Waafghani
17 Desemba 2023Kuondoka kwa ghafla kwa maelfu ya Waafghanistan wasio na vibali kumemwacha Bibi Jawzara, mwanamke mzee wa Pakistani, "akiwa na wasiwasi mkubwa."
Kwa miongo kadhaa, amekuwa akitegemea wahamiaji wa Afghanistan kuhudumia shamba lake katika jimbo la kusini magharibi la Balochistan, ambalo linapakana na Afghanistan.
Lakini baada ya maafisa wa Pakistan kuanzisha kampeni ya kuwafukuza Waafghanistan wapatao milioni 1.7 wasiokuwa na vibali vya kuishi mwezi uliopita, mzee huyo wa zaidi ya miaka 70 amekuwa akihangaika kupata wafanyakazi wenye ujuzi wa kukatia na kurutubisha miti ya tufaha na mizabibu kwenye ardhi yake.
Soma pia: Waafghani wanaofukuzwa Pakistan wakabiliwa na madhila makubwa
"Wakati muhimu wa mbolea umenifikia lakini sina wafanyakazi wa kutosha kwa kazi hii," aliiambia DW. "Wanangu wa kiume na wajukuu wanaishi katika miji kwa ajili ya biashara na elimu, wakimbizi wa Afghanistan walitunza bustani zetu kwa miaka mingi. Lakini sasa walipoondoka ghafla kuepuka kufukuzwa, tunajikuta katika hali mbaya."
Waafghanistan warudi nyumbani baada ya miongo kadhaa Pakistan
Jawzara alikuwa akiajiri watu wa familia tano za Wapashtun wa Afghanistan, ambao walikimbia nchi yao baada ya uvamizi wa Kisoviet mnamo 1979. Wanawake wakimbizi walikuwa wakifanya kazi za nyumbani kwake na wanaume walifanya kazi mashambani, huku mwanamke huyo wa Pakistani na wanawe wawili wakiwasimamia na kuwasaidia.
Hata vizazi vipya katika jumuiya ndogo iliyozaliwa na kukulia Pakistani, walizowea kuishi katika shamba la Jawzara na kumtegemea mwajiri wao huyo kwa chakula, huduma za afya na mahitaji mengine. Lakini ukandamizaji wa hivi karibuni dhidi ya wahamiaji umebadilisha kila kitu.
Soma pia:Wakimbizi 10,000 wa Afghanistan wakimbilia mpaka wa Pakistan
Waafghanistan wengi wasio na vibali nchini Pakistan walikuwa wakiishi katika majimbo ya Balochistan na la kaskazini-magharibi la Khyber Pakhtunkhwa - yote yanayopakana na Afghanistan - na hawakuwahi kuhisi kuwa hati za ukaazi ni muhimu, huku maisha yao yakiwa yamejikita katika maeneo yao.
Mapema mwaka huu, serikali ya Pakistan ilitangaza uwepo wa wahamiaji wasio na vibali kuwa changamoto ya kiusalama na kiuchumi. Mamia ya maelfu tayari wamefukuzwa au waliondoka wenyewe.
Na, licha ya maafisa wa Pakistan kuahidi kwamba wahamiaji halali milioni 2.3 wa Afghanistan walikuwa huru kubaki ilimradi nyaraka zao ni halali, zaidi ya wahamiaji kadhaa wenye nyaraka za ukazi waliamua kurudi nchini mwao.
Walihofia kwamba hivi karibuni Pakistan ingejaribu kuwafukuza pia, na kuonya kwamba mamlaka inaonekana imedhamiria kuwafukuza Waafghanistan wote - wawe wameandikishwa au wasio na nyaraka.
Wafanyakazi wa Afghanistan, waajiri wa Pakistani wastukizwa
Wafanyakazi wa Afghanistan wana sifa ya kutokuwa na gharama kubwa, wenye ujuzi na wachapakazi. Pia wako katika nafasi dhaifu kutokana na kuishi katika ardhi ya kigeni. Kuondoka kwao kwa wingi sasa kumesababisha uhaba wa wafanyakazi katika sekta kama kilimo na madini katika maeneo ya mpakani ya Pakistan.
Soma pia:Je, Pakistan itawafukuza wakimbizi milioni 1.7 wa Afghanistan?
"Maagizo ya wahamiaji [wasio na vibali] kuondoka yamewakuta wafanyakazi wetu wa Afghanistan, pamoja na sisi, bila mandalizi. Wala hawakuwa tayari kiakili kuondoka kwa taarifa ya muda mfupi, na wala hatukuwa na wazo lolote la nini cha kufanya bila wao," alisema Jahangir. Shah, ambaye ana mgodi wa makaa ya mawe katika wilaya ya Duki ya Balochistan.
Waafghan wanaunda asilimia 60 ya wafanyakazi wa Shah. Juhudi za kuwarejesha nyumbani, kwa mujibu wa mmiliki huyo wa mgodi, zilimlazimu kusimamisha shughuli za uchimbaji kwa muda. Hata baada ya kazi kuanza tena kwa zamu zilizopanuliwa, uzalishaji ulikuwa wa polepole sana kwa sababu ya uhaba wa wafanyakazi. Shah anahofia kuwa malengo ya uzalishaji hayatafikiwa.
"Juhudi zetu za kurejea katika hali ya kawaida zinakabiliwa na changamoto, hasa kukosekana kwa wafanyakazi wenye ujuzi," aliiambia DW, na kuongeza kuwa wafanyakazi kutoka maeneo mengine "hawaji licha ya ahadi za malipo bora."
Matatizo kwa Afghanistan
Wapashtun ndiyo kabila kubwa nchini Afghanistan, na mamilioni yao wanaishi pia Pakistan. Sardar Muhammad Shafiq Tareen, Mpashtun na seneta wa mkoa wa Balochistan wa Pakistan, anaonya kwamba karibu asilimia 80 ya wafanyakazi katika migodi na mashamba katika jimbo zima walikuwa watu wa Afghanistan.
Soma pia: Umoja wa Mataifa wasema dola bilioni 5 zinahitajika kuisaidia Afghanistan
Kuhama kwa Waafghanistan pia kutasimamisha utumaji pesa kutoka Pakistan kwenda Afghanistan, na kuathiri maendeleo ya kiuchumi ya Afghanistan, alisema. Nchi hiyo iliyoharibiwa na vita tayari inakabiliwa na mzozo mkubwa kufuatia kuingia madarakani kwa Taliban mwaka 2021.
Tareen alirejea wasiwasi wa wanaharakati wengi na mashirika ya kimataifa, akibainisha kwamba Waafghan walipewa muda mfupi sana wa kurejea nchini mwao licha ya kukaa miaka au miongo katika upande mwingine wa mpaka. Akizungumza na DW, alihoji maelezo ya serikali ya Pakistan kwamba kuondoka mara nyingi kulikuwa kwa hiari.
Hatari kwa sekta ya ndani ya uchimbaji
Vyama mbalimbali vya kisiasa na vyama vya wafanyabiashara vimekuwa vikipinga sera za serikali tangu Oktoba 20 kwa kufanya mgomo katika mji wa mpakani wa Chaman. Wamepinga vizuizi vya visa kufuatia ukandamizaji dhidi ya wahamiaji.
Pir Muhammad Kakar, katibu mkuu wa tawi la Balochistan la Shirikisho la Wafanyakazi wa Pakistani, alisema zaidi ya nusu ya Waafghanistan wanaofanya kazi katika migodi ya jimbo hilo wameondoka, na kusababisha "hali ya uharibifu" kwa sekta ya madini ya ndani, ambayo ndiyo chanzo kikubwa zaidi cha mapato kwa jimbo hilo.
Kakar alisema wamiliki wa migodi hivi karibuni walikutana na Waziri wa Mambo ya Ndani Sarfraz Bugti - mwenyewe mzaliwa wa Balochistan - ambaye aliahidi kuhakikisha kuwa wafanyakazi wa migodi wa Afghanistan hawasumbuliwi. Waziri huyo pia aliahidi sera sahihi kuwezesha wafanyakazi kuendelea na ajira, lakini ahadi hii bado haijatekelezwa, kulingana na Kakar.