1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mashabiki wa soka waingia Poland na Ukraine

4 Juni 2012

Kinyang'anyiro cha soka la mataifa ya bara ulaya - UEFA EURO 2012, kinaanza 8.6.2012 na nchi ya pili itakayokuwa mwenyeji wa dimba hilo Poland, itawakaribisha takribani mashabiki wa kigeni wa soka milioni moja.

https://p.dw.com/p/157j8
Ein Junge holt am Mittwoch (2.5.2012) in Berlin einen Panini-Sticker mit den Maskottchen Slavek und Slavko aus der Stickertüte zur UEFA EURO 2012 in Polen und Ukraine. Foto: Jens Kalaene
Panini-Sticker Slavek Slavko Sammelalbum zur UEFA EURO 2012Picha: picture-alliance/dpa

Viwanja vipya vya michezo vimejengwa, na maeneo makubwa ya mashabiki kutazama mechi kupitia televisheni kubwa yamewekwa tayari kwa uhondo huo. Eneo la katikati mwa mji mkuu Warsaw linalokuwa na shughuli nyingi karibu na Kasri la Utamaduni limepewa jukumu jipya.

Kuna majukwaa mawili yaliyoezekwa na kuwekwa televisheni sita kubwa ambazo zitatumiwa na mashabiki 100,000 umati ambao ni mkubwa zaidi nchini Poland na Ukraine. Miji mingine ya Poland itakayoandaa dimba hilo mji wa Bandari wa Gdansk, mji wa Kusini Magharibi Wroclaw na ule wa Magharibi Poznan pia inaendelea na mipango ya mwisho mwisho. Hoteli na vyumba vya kulala pia vimefurika wageni wengi.

Ujerumani na matumaini
Timu ya taifa ya Ujerumani imewasili nchini Poland kwa mashindano ya UEFA EURO 2012 ikiwa na kiungo wake muhimu Bastian Schweinsteiger ambaye ameripotiwa kuwa katika hali nzuri kiafya. Mkufunzi wa timu hiyo Joachim Löw yuko na matumaini makubwa ya kusajili matokeo bora.

Kikosi cha taifa kitakachoshiriki dimba la UEFA EURO 2012
Kikosi cha taifa kitakachoshiriki dimba la UEFA EURO 2012Picha: picture alliance / dpa

Timu ya Ujerumani itakuwa na kambi yake katika mji wa Gdasnk, nchini Poland, katika kipindi kizima cha dimba hilo, litakaloanza Ijumaa hii huku fainali ikichezwa mjini Kiev tarehe mosi Julai nazo mechi zote za kundi B zikichezwa nchini Ukraine.

Wajerumani wamekuwa na changamoto kadhaa wakati wa maandalizi yao ya mwisho baada ya kushindwa na Switzerland magoli 5 – 3 katika mchuano wa kujipima nguvu, naye kiungo Bastian Schweinsteiger akiendelea kupona jeraha lake la kifundo cha mguu. Ujerumani ni miongoni mwa timu zinazopigiwa upatu kabla ya kung'oa nanga kwa kivumbi hicho, na wataanza kampeni yao Jumamosi hii dhidi ya Ureno huku Schweinsteiger akipewa idhini ya kucheza. Huyu hapa kocha

Löw alenga taji lake la kwanza

Joachim Löw ambaye analenga kutwaa taji lake la kwanza kama kocha wa Ujerumani baada ya kuifikisha timu hiyo hadi fainali ya UEFA EURO 2008 na nusu fainali Kombe la Dunia mwaka wa 2010. Amesema wamefanya vyema mazoezi, na wana fuiraha kwamba dimba tayari linaanza.

Joachim Löw aendelea kuyanoa makali ya vijana wake
Joachim Löw aendelea kuyanoa makali ya vijana wakePicha: picture-alliance/dpa

Löw angali na maamuzi kadhaa ya kufanya baada ya wachezaji Mario Gotze wa Borussia Dortmund, Per Mersacker wa Arsenal, mshambuliaji wa Lazio Miroslav Klose na Schweinsteiger wote kurejea kutoak mkekani. Ikiwa Schweinsteiger hatapona vyema kwa wakati unaofaa, mwenzake wa klabu ya Bayern Munich Toni Kroos huenda akashirikiana na Sami Khedira wa Real Madrid katika safu ya kati. Nahodha Philip Lahm anatarajiwa kuanza kama beki wa kushoto na mwenzake wa Bayern Jerome Boateng akiwa upande wa kulia.

Löw anahitaji kuchagua baina ya Mats Hummels wa Dprtmund, Holger Badstuber wa Bayern na Mertesacker wa Arsenal kuchukua nafasi mbili za bei wa kati. Mshambuliaji wa pekee atakuw Mario Gomez wa Bayern.

Mfumo wa 4-2-3-1 kutawala
Kiufundi, mfumo wa 4-2-3-1 huenda ukatawala katika kinyang'anyiro hicho jinsi tu ilivyokuwa katika fainali za kombe la dunia la mwaka wa 2010, ambapo timu tatu za ulaya zilizofika nusu fainali yaani Ujerumani, Uholanzi na mabingwa Uhispania, zote zilitumia mfumo huo.

Timu 16 zitakabana koo kutafuta ubingwa wa dimba la UEFA EURO 2012
Timu 16 zitakabana koo kutafuta ubingwa wa UEFA EURO 2012

Timu zote hizo tatu zinatarajiwa kusalia na mfumo huo, ijapokuwa mchezo wao utatofautiana. Uhispania inafahamika na mbinu yao gonga gonga maarufu kama tiki taka, huku nazo Ujerumani na Uholanzi zikitegemea mbinu yao ya mashambulizi makali.

Dhamira ya mkufunzi Laurent Blanc ya kuwajaza washambuliaji katika timu yake ina maana kuwa Ufaransa huenda ikasalia na mfumo wake wa 4-3-3 ambao ulitumiwa katika mchuano wa hivi majuzi wa kujinoa makali ambapo waliwashinda Serbia magoli mawili kwa sifuri.

Uingereza huenda ikawa mojawapo ya timu chache zinazoongoza kucheza na washambuliaji wawili wa kati, ikizingatiwa kuwa kocha mpya Roy Hodgson anaupenda mfumo wa 4-4-2. hata hivyo kutokana na pengo litakalowachwa na Wayne Rooney katika mechi mbili za kwanza, kulimhimiza Hodgson kujaribu mfumo wa 4-4-1-1 ambapo Ashley Young aliwachwa mbele kama mshambuliaji wa pekee.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA/Reuters
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman