1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mpango wa kufunga jela ya Guantanamo warefushwa

11 Novemba 2015

Juhudi za rais Barack Obama kulifunga gereza la Guantanamo zimeingia katika utata mkubwa. Baraza la Seneti la nchi hiyo jana lilipitisha mswada, unaofahamika kama sheria inayotoa ulinzi kwa taifa

https://p.dw.com/p/1H3qC
Symbolbild Guantanamo
Picha: Getty Images/J. Moore

Seneti ilipitisha mswada huo kwa wingi mkubwa kura 91 dhidi ya 3. Mswada huo unarefusha marufuku ya kuwahamisha wafungwa waliobaki 112 kutoka gereza la Guantanamo kwenda Marekani.

Uungwaji mkono wa mswada huo una maana kwamba baraza la Seneti la Marekani linaweza kirahisi kuzuwia kura ya turufu ya rais.

Rais Obama alikuwa ameupinga mswada wa awali kwa sababu ya lugha ya Guantanamo na kwa sababu ulipunguza gharama za matumizi jeshini bila pia kulegeza vizuizi kwa gharama za matumizi ya ndani.

Mswada huo wa ulinzi, ambao ulitathminiwa ili kuakisi mpango wa bajeti ya miaka miwili ulioidhinishwa na Obama kuwa sheria wiki iliyopita ambao ulitatua mgogoro wa matumizi, ulipita kwa urahisi bungeni wiki iliyopita.

Kura za kuipinga sheria hiyo inayotoa ulinzi kwa taifa, katika Kiingereza National Defense Authorization Act – NDDA, ni pigo kwa ahadi ya Obama kulifunga gereza la Guantanamo kabla ya kuondoka madarakani mwaka wa 2017.

USA US-Senat stimmt für Folter-Verbot bei Verhören John McCain
Seneta wa Republican John McCainPicha: Reuters/J. Ernst

Pamoja na kurefusha marufuku ya kuwahamishia Marekani wafungwa wa Guantanamo, mswada huo unapendekeza masharti au vizuizi vipya wa kuwahamishia mataifa ya tatu, yakiwemo Libya, Syria, Yemen na Somalia. Hata wabunge wanaotaka kulifunga gereza la Guantanamo, kama vile Seneta wa Republican John MCain, wameelezea kusikitishwa kwao kwamba Obama, ambaye amekuwa madarakani tangu 2009, hajatuma bungeni mpango wake wa kulifunga.

Utawala wa Obama unatarajiwa kuwasilisha mpango wake baadaye wiki hii. Utapata pingamizi kali Bungeni na kumekuwa na mazungumzo kwamba huenda akaamua kutumia amri ya rais kulifunga gereza hilo.

Wazo hilo linawakasirisha Warepublican, wengi wao ambao wanaichukulia Guantanamo kuwa muhimu katika kuwazuia washukiwa wa kigeni wa ugaidi. Obama na wabunge wanaounga mkono kufungwa kwa jela hilo, wengi wao Wademocrat wenzake, wanaliona kuwa picha yenye kuharibu inayoonyesha mateso na kuzuiwa washukiwa bila kuwafungulia mashtaka.

Kiongozi wa Democrat katika baraza la Senate Harry Reid amesema sasa ni juu ya Obama kuamua namna ya kusonga mbele na suala hilo.

Mwandishi: Bruce Amani/reuters
Mhariri:Mohammed Abdul-rahman