1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maafisa wa Marekani kuhojiwa kuhusu mauaji ya Khashoggi

28 Novemba 2018

Maseneta ambao hawajaridhishwa na jibu la serikali ya Marekani kuhusu Saudi Arabia kufuatia mauaji ya mwandishi habari Jamal Khashoggi wanatarajiwa kuwahoji maafisa wakuu wa utawala wa Rais Donald Trump leo, Novemba 28

https://p.dw.com/p/394bA
Saudi Arabien, Kronprinz - Mohammed bin Salman
Picha: Reuters/C. Platiau

Mahojiano hayo yatafanyika katika mkutano wa faragha ambao utabaini umbali ambao Bunge litakwenda kuiadhibu Saudi Arabia ambayo imekuwa mshirika wa karibu wa Marekani kwa muda mrefu. Kiongozi wa wengi katika baraza Seneti Mith McConnell amesema aina fulani ya majibu yanahitajika kutoka Marekani kuhusu jukumu la Wasaudi katika mauaji ya Khashoggi. Mengi yatategemea kile maseneta watayasikia kutoka kwa Waziri wa Ulinzi Jim Mattis na Waziri wa Masuala ya Ndani wa Marekani Mike Pompeo.

Mapema mwaka huu maafisa wa serikali ya Marekani walifanikiwa kukwamisha juhudi za Senate dhidi ya mgogoro wa muungano unaoongozwa na Saudi Arabia nchini Yemen. Lakini maseneta hao wamekasirishwa na majibu kuhusu mauaji ya Jamal Khashoggi, na hasa suala kwamba hakuna yeyote katika idara ya ujasusi atakayehudhuria kikao cha leo.

Seneta wa Virginia Magharibi, Joe Manchin, mmoja wa maseneta kumi wa Democrats ambaye awali alikataa kujiunga na maseneta wengine dhidi ya Wasaudi, jana Jumanne alisema kwamba anatathmini upya msimamo wake. Wakati hayo yakijiri, Mrithi wa Ufalme nchini Saudi Arabia Mohammed bin Salman amewasili mjini Buenos Aires kwa mkutano wa G20, huku akilenga kupuuza unyanyapaa anaokabiliwa nao kufuatia mauaji ya Khashoggi.

Saudi-Arabiens Kronprinz MbS und Erdogan
Picha: picture-alliance/AA/K. Ozer

Salman alilakiwa kwenye uwanja wa ndege na Waziri wa Masuala ya Nje wa Argentina Jorge Faurie kulingana na shirika la habari la Argentine. Inaarifiwa kuwa huenda akakutana na Rais wa Uturuki Reccep Tayyip Erdogan kando ya mkutano huo. Huu ndio utakuwa mkutano wao wa kwanza tangu kuuawa kwa Khashoggi katika ofisi ya ubalozi mdogo wa Saudi Arabia mjini Istanbul tarehe 2 Oktoba mwaka huu. Wakati huo huo Argentina inatarajiwa kutoa uamuzi wa iwapo itamchunguza mrithi huyo wa ufalme kufuatia mauaji hayo na uhalifu wa kivita nchini Yemen.

Juzi Jumatatu, mkuu washirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch, Kenneth Roth, aliitaka Argentina kuanzisha uchunguzi huo. Saudi Arabia imekuwa ikipokea ukosoaji wa kimataifa kufuatia mauaji ya Jamal Khashoggi ambaye aliuliwa na kukatwakatwa katika kile Saudi Arabia imekitaja kuwa oparesheni mbaya, ingawa uchambuzi wa Shirika la Ujasusi ya Marekani, CIA, iliyotolewa kwa vyombo vya habari vya Marekani umeonekana kumhusisha Mohammed bin Salman.

Mwandishi: Sophia Chinyezi/AFPE/APE

Mhariri: Mohammed Khelef