Marufuku ya maandamano Kisumu yapingwa
4 Agosti 2017Mashirika yasiyo ya kiserikali mjini Kisumu yamepinga hatua ya kamati ya usalama ya mji huo kupiga marufuku maandamano yote kabla na baada ya uchaguzi mkuu utakaofanyika Jumanne ijayo, ikiwa sehemu ya mkakati wa kuepusha vurugu na uharibifu wa mali wakati wa kura, jambo ambalo imedai hutokea wakati wa maandamano.
Kaunti ya Kisumu imetajwa kuwa kati ya maeneo yaliyo na uwezekano mkubwa wa kuzuka vurugu wakati wa uchaguzi mkuu ujao. Hii inafuatia fujo zilizojitokeza katika chaguzi za awali na haswa wa mwaka 2007, zilizozuka baada matokeo yaliyotangazwa kuibua utata.
Tahadhari ya kiusalama
Mali ya thamani kubwa iliharibika kwa kuporwa na ama kuteketezwa, na maafa mengi yalitokea, huku jamii ambazo si za hapa zikilazimishwa kuhama na mali yao kutwaliwa.
Mambo haya yameilazimu kamati ya usalama kuweka mikakati mingi ya usalama na mkuu wa kamati hii ambaye pia ni kamishna wa Kaunti ya Kisumu, Mohammed Maalim, kuonya hivi kuhusu maandamano: "Tutatumia rasilimali zote zilizopo kuhakikisha kuwa hakuna maisha yatakayopotezwa au mali kuharibika, tumepiga marufuku maandamano yote kwa hii kaunti ya Kisumu na hakuna anayetakiwa kuingiza siasa kwa hili."
Kauli hii hata hivyo imezua utata na mashirika yasiyo ya kiserikali kwa kuongozwa na Mwenyekiti wa chama cha Wakaazi wa Kisumu, Audi Ogada, kusema haikubaliki.
Idadi kubwa ya askari
Kadhalika wameelezea hofu yao kuhusu kutumwa kwa idadi kubwa ya askari kulinda usalama wakati wa kura katika mji wa Kisumu na ukanda huu wa ziwa kwa jumla na kuwaomba wananchi hapa kupiga kura kwa amani.
Ofisi nyingi kuanzia leo zimetoa nafasi kwa wafanyakazi kujiandaa kupiga kura siku ya Jumanne na vituo vya mabasi vimejaa wasafiri wengi wanaosafiri kwenda walikojiandikisha, huku wengine wakisema wanachukua tahadhari za usalama.
Mwandishi: John Marwa/DW Kisumu
Mhariri: Mohammed Khelef