1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Martin Schulz mgombea wa ukansela wa SPD

25 Januari 2017

Chama cha SPD cha Ujerumani kimemtagaza spika wa zamani wa bunge al Ulaya Martin Schulz kuwa mgombea wake wa ukansela na pia mwenyekiti mpya wa chama hicho.

https://p.dw.com/p/2WMM4
Deutschland  Schulz erhebt Führungsanspruch der SPD
Picha: Reuters/F. Bensch

Tangazo hilo lilikuja baada ya mwenyekiti wa  chama cha SPD ambaye pia ni naibu kansela Sigmar Gabriel kuwashangaza waangalizi kwa kusema kwamba angekaa pembeni na kumpisha Schulz, akikiri kuwa nafasi yake ya kumshinda Merkel katika uchaguzi wa Septemba 24 ilikuwa finyu.

"Martin Schulz ndiye atakuwa mgombea wa SPD kwa nafasi ya Kansela katika uchaguzi mkuu mwaka huu. Kamati ya uongozi ilipiga kura kwa sauti moja kupendekeza jina lake kwa mkutano mkuu wa chama, ambao utafanya maamuzi yake ya mwisho siku ya Jumapili," alisema Gabriel katika mkutano wa waandishi habari mjini Berlin.

 Martin Schulz pia atachukuwa uenyekiti wa chama cha SPD, alisema Gabriel na kuongeza kuwa suala hilo limependekezwa na yeye, Olaf Scholz na Honolare kraft kwa kamati ya uongozi na ikalikubali kwa sauti mmoja.

Deutschland  Schulz erhebt Führungsanspruch der SPD
Martin akitabasamu wakati yeye na Sigmar Gabriel wakiwa katika mkutano na waandishi habari mjini Berlin.Picha: Reuters/F. Bensch

Ashindana na Merkel kwa umaarufu

Schulz mwenye umri wa miaka 61 ambaye wiki iliyopita ndiyo alihitimisha uongozi wa miaka mitano kama spika wa bunge la Ulaya, alisema katika mkutano huo na waandishi habari kwamba amekubali uteuzi huo, kwa fahari na unyenyekevu. Ingawa muungano wa Merkel wa CDU na CSU uko mbele ya SPD, uchunguzi wa karibuni wa maoni ya wapiga kura unaonyesha kuwa umaarufu wa Schulz ambaye ni mtu mashuhuri nchini Ujerumani unashindana na wa Merkel kwa ngazi ya mtu binafasi.

Kuingia kwake katika kinyang'anyiro hicho kunaweza kumuumiza kichwa kansela Merkel mnamo wakati chama chake tayari kinakabiliwa na kishindo kutoka kwa chama cha siasa kali za kizalendo za mrengo wa kulia cha Alternative für Deutschland - Chama mbadala kwa Ujerumani AfD, ambacho kimetumia vizuri hasira za wananchi kuhusu sera ya Merkel kuhusu wakimbizi kujiongezea umaarufu.

Uchunguzi wa maoni kwa sasa unaonesha kuwa chama cha Merkel cha CDU kina nafasi kubwa ya kushinda uchaguzi wa kitaifa kwa karibu asilimia 37, kikifuatia kwa mbali na SPD yenye asilimia karibu 20, ikiwa imedhoofishwa na miaka kadhaa ya kutong'aa wakiwa washirika wadogo katika serikali ya muugano ya Merkel. Chama cha mrengo mkali wa kulia cha AfD wakati huo kina karibu asilimia 15 kulingana na uchunguzi huo wa maoni.

EU-Gipfel in Brüssel
Kansela Angela Merkel akiwa na Martin Schulz mjini Brussels Desemba 15, 2016.Picha: picture-alliance/dpa/O. Hoslet

Kurudi nyumbani kunakopendeza

Kuteuliwa kwa Schulz kunaashiria kurejea nyumbani kunakopendeza kwa mstaafu wa Umoja wa Ulaya, aliyetangaza miezi miwili iliyopita kwamba anaondoka Brussels kujitosa katika siasa za Ujerumani. Licha ya kutokuwepo kwa muda mrefu, Schulz ameendelea kuwa mtu maarufu nchini Ujerumani, akionekana mara kwa mara katika vyombo vya habari, huku akijiweka mbali na siasa za kila siku za ndani.

Umaarufu wa Gabriel, aliyeiongoza SPD tangu mwaka 2009 na ambaye pia ni waziri wa uchumi wa Ujerumani umeshuka kwa kiasi kikubwa katika miaka ya karibuni, na wakosoaji wanasema hakuwahi kutoa uongozi mbadala kwa Merkel, aliyeingia madarakani mwaka 2005.

Merkel mwenye umri wa miaka 62, alitangaza mwezi Novemba mwaka uliopita kuwa atawania muhula wa nne, lakini alikiri kuwa uchaguzi wa mwaka huu utakuwa mgumu zaidi kuliko mwingine wowote aliowahi kugombea.

Mwandishi: Sabine Kinkartz/Iddi Ssessanga

Mhariri: Josephat Charo