Martin Schulz kuwaongoza wana SPD kutwaa kiti cha kansela
3 Aprili 2017Akiwa na umri wa miaka 61 spika huyo wa zamani wa bunge la ulaya anazidi kupata umashuhuri na kwa wiki kadhaa sasa taasisi za uchunguzi wa maoni ya umma zinamweka bega kwa bega na kansela Merkel aliyeko madarakani tangu mwaka 2005. Itafaa akusema hapa kwamba mapema mwaka huu SPD kilitajikana kuwa nyuma ya kansela Merkel kwa pointi 15.
Wakipata moyo kutokana na hali hiyo wafuasi wa SPD wamemchagua kwa sauti moja, mia kwa mia, Martin Schulz awe mwenyekiti wa chama chao, tukio ambalo halijawahi kushuhudiwa katika historia ya chama hicho kikongwe kabisa cha kisiasa cha Ujerumani.
Baada ya kuwasahukuru wana SPD Martin Schulz amesema:"Kuanzia sasa yanaanza mapambano ya kulifikia lengo letu nalo ni kurejea kuwa chama kikubwa zaidi humu nchini na kuipatia nchi hii kanasela mpya."
Chama cha SPD kina pointi sawa na CDU/CSU
Amerithi wadhifa uliokuwa ukishikiliwa na Sigmar Gabriel, waziri wa sasa wa mambo ya nchi za nje aliyelazimika kuachia ngazi kutokana na kushindwa kupata imani ya wapiga kura.
Kabla ya uchaguzi mkuu wa Septemba 24 ambapo SPD wanasemekana kuwa sawa na CDU/CSU kila upande ukiwa na zaidi ya asili mia 30, chaguzi tatu za majimbo zitafanyika, chaguzi zinazoangaliwa kama kipimo cha uchaguzi mkuu unaokuja.
Katika jimbo dogo kabisa la Saar ambako uchaguzi utaitishwa wiki moja kutoka sasa,SPD wanatishia kuwatimua madarakani CDU wanaolitawala jimbo hilo la magharibi tangu miaka 18 iliyopita.
Martin Schulz anaangaliwa kama mtoto wa umma
Martin Schulz ni sura mpya katika medani ya kisiasa nchini Ujerumani na kuteuliwa kwake kugombea kiti cha kansela kunatokea katika wakati ambapo hisia za kuchoshwa na kansela Merkel zinaonyesha kuzagaa" anasema mtaalam wa masuala ya kisiasa Michael Spreng katika mahijiano na gazeti la Süddeutsche Zeitung.
Wasifu wa aina pekee wa mwanasiasa huyo aliyekumbwa na mitihani ya kila aina katika ujana wake, ukichanganyika na sifa za mwenye kusema kweli yanamfanya aangaliwe kuwa mtoto wa umma.
Wana SPD wanaamwangalia Martin Schulz kama ngao dhidi ya siasa kali za mrengo wa kulia."Katika wakati huu wa vitisho vya mrengo wa kulia na wimbi la wasiopenda demokrasia, naamini bora kujitambulisha na chama cha SPD, kama kitambulisho muhimu cha demokrasia. Na ndio maana nimejiunga na SPD tangu january mosi."
Katika mkutano wao mkuu jana mjini Berlin wana SPD wamedhihirisha moja kwa moja kumuunga mkono mgombea wa chama cha En March,Emmanuel Macron nchini Ufaransa ambae jina lake lilitajwa sana na kushangirwa.
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/AFP
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman