MARSEILLE Msaada wa chakula wapelekwa Niger
21 Julai 2005Ndege ya kwanza iliyobeba tani 18 za msaada wa chakula kinachohitajika kwa dharura nchini Niger, imeondoka kutoka mjini Marseille, Ufaransa, kuelekea mjini Maradi, kazkazini mashariki mwa Niger. Chakula hicho kitapelekwa katika maeneo yaliyoathiriwa na njaa kutumia ndege nyengine ndogo, katika oparesheni iliyodhaminiwa na makampuni kadhaa makubwa ya kimataifa.
Kiongozi anayeshughulikia mipango ya misaada katika umoja wa mataifa, Jan Egeland, ametoa mwito wadhamini wajitokeze na michango yao ili kuwasaidia raia milioni 3.5 wanaoteseka kwa njaa nchini Niger, wakiwemo watoto elfu 800. Shirika la misaada la Oxfam limeitaka jamii ya kimataifa kufanya haraka kuwasaidia raia hao, kwani hakuna matumaini ya mavuno katika kipindi cha miezi mitatu ijayo.