Mark Rutte ashinda uchaguzi mkuu Uholanzi
16 Machi 2017Sarafu ya Euro imepanda kufuatia matokeo ya uchaguzi wa jana nchini Uholanzi, matokeo yaliyodhihirisha ushindi wa Mark Rutte, licha ya kupoteza baadhi ya viti ikilinganishwa na uchaguzi wa mwaka 2012. Baada ya matokeo ya awali kutangazwa, mhafidhina huyo anaefuata siasa za kiliberali amesema waholanzi baada ya kura ya maoni ya Brexit na uchaguzi wa Marekani wameamua kuzuwia hisia za uzalendo wa uwongo: "Ni siku muhimu kwa Ulaya. Nimeshazungumza kwa simu na viongozi kadhaa wa Ulaya, mara baada ya waholanzi, kupinga hisia za uzalendo wa uwongo, baada ya kura ya Brexit na uchaguzi wa Marekani.
Mpinzani wake, mfuasi wa siasa kali za kizalendo, mpinzanai mkubwa wa dini ya kiislam na Umoja wa Ulaya, Geert Wilders anayataja matokeo ya uchaguzi kuwa ni ya kuridhisha. Anaashiria chama chake cha Uhuru PVV kitaingia madarakani uchaguzi mwengine utakapoitishwa.
Wajerumani wampongeza Mark Rutte
Baada ya sehemu kubwa ya kura kuhesabiwa chama cha Rutte VVD kimejikingia viti 33 kati ya 150 vya bunge, chama cha siasa kali za mrengo wa kulia PVV kimekamata nafasi ya pili kwa kupata viti 20-viti vitano zaidi ikilinganishwa na uchaguzi mkuu uliopita.
Wanasiasa wa Ujerumani wameyakaribisha matokeo ya uchaguzi huo wa Uholanzi. Kansela Angela Merkel amezungumza kwa simu mara baada ya matokeo kutangazwa jana usiku na kumpongeza Mark Rutte. Msemaji wa serikali ya Ujerumani, Steffen Seibert amemnukuu kansela akisema, "anasubiri kwa hamu kuendeleza ushirikiano wa kirafiki pamoja na majirani, wana Umoja wa Ulaya. Naye kiongozi wa ofisi ya kansela Peter Altmeier ameitaja Uholanzi kuwa ni mabingwa."
Monica Braun ni mkaazi wa jimbo jirani na Uholanzi, la North Rhine Westphalia. Yeye anasema: "Sijui kama matokeo hayo yatakuwa na uzito wowote kwa uchaguzi wa Ufaransa. Lakini nina uhakika matokeo ya uchaguzi wa Uholanzi yatakuwa na umuhimu mkubwa kwa uchaguzi mkuu nchini Ujerumani. Naamini matokeo ya uchaguzi wa Uholanzi ni muhimu kwa Umoja wa Ulaya.
Marine Le Pen hakusema chochote baada ya rafiki yake Wilders kushindwa
Mgombea kiti cha rais nchini Ufaransa, Emmanuel Macron amesifu matokeo ya uchaguzi wa Uholanzi akisema "ni ushindi kwa wenye kupigania maendeleo".
Kiongozi wa siasa kali za mrengo wa kulia nchini Ufaransa, Marine Le Pen bado hajasema chochote kuhusu kushindwa kwa mshirika wao Geert Wilders.
Wakuu wa vyama vya VVD, Christian Democrats na walinzi wa mazingira D66, wanatarajiwa kukutana baadae leo jioni kuzungumzia uwezekano wa kuunda serikali ya muungano.
Mwandishi: Hamidou Oummilkheir/AP/Reuters
Mhariri: Yusuf Saumu