Marine Le-Pen atwaa ushindi Ufaransa
7 Desemba 2015Uchaguzi huo umefanyika wakati nchi hiyo ikiwa katika sheria ya hali ya dharura iliyowekwa wiki tatu zilizipita baada ya kufanyika mashambulizi ya wenye itikadi kali yaliyosababisha watu 130 kuuwawa mjini Paris.
Chama cha siasa kali za mrengo wa kulia FN kinachoongozwa na Marine Le Pen ambaye kitaaluma ni mwanasheria kimejipatia ushindi huo mkubwa kabisa wa kiasi asilimia 28 kote Ufaransa na kuibuka kidedea katika orodha ya vyama vilivyoingia kwenye uchaguzi huo katika majimbo alau sita kati ya 13 kwa mujibu wa makadirio ya mwisho ya matokeo yaliyotolewa na wizara ya mambo ya ndani.
Ushindi huo umevunja rekodi ya asilimia 40 iliyowekwa na chama hicho huko nyuma katika majimbo hayo,matokeo ambayo yametokana zaidi na hasira za wapiga kura kuhusiana na suala la kudumaa kwa uchumi na khofu ya usalama inayohusishwa na mgogoro wa wimbi la wakimbizi barani Ulaya.Marine Le Pen ameyapokea matokeo hayo kwa furaha kubwa na kusema ni matokeo makubwa akisema yamedhihirisha chama chake cha FN ni nambari moja na hakina mpinzani nchini Ufaransa.
"Watu wa Ufaransa wamejieleza .Na kwa mujibu watu wa nchi hii,Ufaransa inanyanyua kichwa.Matokeo ya uchaguzi huu yanathibitisha kile ambacho kilionekana katika chaguzi zilizopita lakini waangalizi rasmi bado hawakutaka kukitambua . FN hakina mpinzani na ndio chama cha Ufaransa,wakati ambapo hakina uwakilishi imara bungeni''
Muungano wa vyama vya mrengo wa kulia vimejizolea asilimia 27 kwa mujibu wa makadirio ya matokeo rasmi wakati chama tawala cha kisosholisti na washirika wake wakijipatia asilimia 23.5 ya kura.Uchaguzi huo wa Jumapili ulifanyika usalama ukiwa umeimarishwa kwa kiwango cha juu kufuatia mashambulizi mabaya ya kigaidi kuwahi kuikumba Ufaransa.Ni matukio hayo ya ugaidi yamekipa nguvu kubwa chama cha Marine Le Pen FN ambacho kinapinga uhamiaji na wakimbizi na mara nyingi kinatoa ujumbe unaoupinga uislamu .
Kiasi nusu ya wapiga kura milioni 45 waliojikindikisha walishiriki upigaji kura hapo jana.Chama chochote kinachoungwa mkono na asilimia 10 katika duru ya mwanzo ya uchaguzi kina haki ya kusimamisha wagombea wake katika duru ya pili ya uchaguzi ambao utafanyika Jumapili ijayo.Makadirio ya matokeo ya mwisho yanaonesha Le Pen mwenye umri wa miaka 47 anaongoza kwa asilimia 40.5 ya kura katika jimbo la kaskazini la Calis-Picardie ambalo linakabiliwa na hali mbaya ya uchumi na ambalo awali lilikuwa ngome ya mrengo wa kushoto.
Mpwa wake Marechal-Le Pen pia alifanya vizuri katika jimbo la Kusinimashariki lenye umaarufu mkubwa kutokana na fukwe zake za bahari zinazopendeza.Kiongozi wa chama cha sosholisti Jean-Christophe Cambadelis amesema chama chake hakitosimamisha mgombea katika duru ya pili ya uchaguzi katika majimbo ambayo Le Pen na mpwa wake wameongoza ili kukizuia chama cha FN.Kufuatia matokeo ya uchaguzi wa Jumapili gazeti la mrengo wa kulia linalotoka kila siku Le Figaro na lile la kikomunisti L'Humanite yote yametoka na kichwa kinachosema(Ni mshtuko) wakati gazeti la mrengo wa kushoto Liberation likionya kwa kuandika''yanakuja''Umaarufu wa rais Hollande umepanda kiasi kutokana na msimamo mkali aliochukua tangu mashambulizi ya Novemba 13 mjini Paris ingawa chama chake kimeshindwa na FN na mrengo wa kulia wa siasa za wastani.
Mwandishi:Saumu Mwasimba
Mhariri:Abdul-Rahman Mohammed