Marekani yaweka vikwazo vipya dhidi ya Venezuela
2 Machi 2019Siku moja baada ya Urusi na China kupiga kura ya turufu dhidi ya azimio la Marekani na Ulaya katika baraza la Usalama la Umoja wa mataifa ambalo lilitaka kufikishwa misaada bila vizuwizi, Marekani ilisema inawalenga maafisa sita wa jeshi la Venezuela kwa kuzuwia msafara ulioongozwa na Marekani mwishoni mwa juma lililopita.
Watu wanne waliuwawa katika vurumai iliyotokea wakati majeshi ya Maduro yalipozuwia tani 178 za mchele , maharage na vyakula vingine kuingia nchini humo kupitia Colombia. Kiongozi huyo wa Venezuela amesema msaada huo ni njama za uvamizi zinazoongozwa na Marekani.
"Tunaweka vikwazo dhidi ya wanajeshi wa jeshi la usalama la Maduro kujibu ghasia za ukandamizaji, vifo pamoja na hatua ya kuchoma moto vyakula na madawa vilivyokuwa vinapelekwa kwa wagonjwa na wale ambao hawana chakula nchini Venezuela," waziri wa fedha Steven Mnuchin amesema katika taarifa.
Wanajeshi 6 walengwa
Watu hao sita ni pamoja na meja jenerali Richard Jesus Lopez Vargas, kamanda wa jeshi la ulinzi la taifa. Vikwazo hivyo vinazuwia mali zozote zilizoko nchini Marekani na kutoa adhabu kwa shughuli zote za kifedha nchini Marekani zitakazofanywa na maafisa hao.
Marekani pia imeondoa visa kwa maafisa 49 wa Venezuela pamoja na familia zao, wizara ya mambo ya kigeni imesema.
Kiongozi wa upinzani wa Venezuela Juan Guaido , ambaye Marekani inamtambua kuwa rais wa mpito , alikuwa na matarajio ya kuweza kuingiza shehena ya misaada nchini Venezuela, ambayo Marekani imeratibu pamoja na Colombia na Brazil.
Guaido amesema watu 300,000 huenda wakafa njaa bila ya kuingizwa misaada nchini Venezuela. Umoja wa mataifa unasema Wavenezuela milioni 2.7 wameikimbia nchi hiyo tangu mwaka 2015 wakati taifa hilo lenye uchumi wa kisoshalisti ulipoporomoka, kutokana na kupungua kwa mahitaji muhimu kwa watu.
Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe