Majeshi ya Marekani yawaua wanajihadi wa Al-Qaeda Syria
17 Machi 2017Kundi linalofuatilia haki za binadamu nchini Syria limesema vifo vingi vilivyotokea katika shambulio la jana jioni katika kijiji cha Al-Jineh kaskazini mwa jimbo la Aleppo vilikuwa ni vya raia.
Muungano wa jeshi unaoongozwa na Marekani umekuwa ukishambulia kwa mabomu makundi ya jihadi katika nchi iliyokumbwa na vita ya Syria tangu mwaka 2014, huku mamia ya raia wakiuuawa bila kukusudiwa ndani ya nchi hiyo na nchi jirani ya Iraq.
Kanali John J. Thomas ni msemaji wa Kamandi kuu ya Jeshi la Marekani katika eneo la Mashariki ya Kati. "Hatukuulenga msikiti, lakini jengo tulilolilenga lilikuwa ndio sehemu ambapo mkutano ulifanyika, na lilikuwa hatua 50 kutoka ulipo msikiti," amesema Kanali Thomas.
Kwa mujibu wa taarifa ya kamandi hiyo, "majeshi ya Marekani yalitekeleza mashambulizi ya angani dhidi ya kundi la Al-Qaeda na kuwaua magaidi kadhaa."
Hata hivyo baadae msemaji wa kamandi alitoa ufafanuzi kwamba eneo ambako mashambulizi hayo yamefanyika halijulikani lakini imeripotiwa kuwa ni tukio moja na lile la kuushambulia msikiti katika kijiji cha al-jineh, mjini Aleppo na kusema kwamba itafanya uchanguzi wa tukio hilo.
Mkuu wa shirika la kutetea haki za binadamu la nchini Syria Rami Abdel Rahman amenukuliwa akisema zaidi ya watu 100 wamejeruhiwa na kwamba wengi bado wamekwama chini ya msikiti ulioharibiwa.
Kijiji hicho cha Al-Jineh kinadhibitiwa na makundi ya kiislamu. Mmoja wa wakazi wa kijiji hicho Abu Muhammed ameliambia shirika la habari la AFP kuwa kulisikika mripuko mkubwa wakati msikiti uliposhambuliwa na kwamba ilikuwa muda mfupi baada ya swala.
"Niliona miili 15 na miili mingi katika eneo la ebris mara nilipoawasili. Hatukuweza kutambua baadhi ya mili," alisema Abu Muhammed.
Wakati huo huo jeshi la Syria limetoa taarifa hii leo Ijumaa ya kuzitungua ndege za Israel wakati zilipokuwa zikifanya mashambulizi ya alfajiri karibu na mji uliogeuka kuwa jangwa wa Palmyra. Taarifa ya jeshi hilo iliyotolewa na shirika la habari la taifa SANA inasema ndege nyingine zimekimbia. Jeshi la anga la Israel awali lilisema kwamba limetekeleza mashambulizi kadhaa nchini Syria usiku kucha lakini hakuna ndege yao hata moja iliyoshambuliwa na jeshi la Syria.
Zaidi ya watu laki tatu wameuawa Syria tangu kuanza kwa mgogoro wa kuipinga serikali miaka sita iliyopita. Usitishaji wa mapigano baina ya vikosi vya serikali na makundi ya waasi wasio wanajihadi yaliratibiwa na Uturuki anayewaunga mkono waasi pamoja na Urusi aliye mshirika wa utawala wa Syria mnamo mwezi isemba, lakini mapigano bado yangali yanaendelea.
Mwandishi: Sylvia Mwehozi/AFP
Mhariri: Iddi Ssessanga