1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yawarudisha zaidi ya wahamiaji 50 kutoka Haiti

Hawa Bihoga
19 Aprili 2024

Marekani imewarudisha zaidi ya wahamiaji 50 kutoka nchini Haiti ambayo inakabiliwa na ongezeko la ghasia za magenge ya uhalifu katika siku za hivi karibuni.

https://p.dw.com/p/4ewpr
Haiti, Port-au-Prince | Polisi wakiwa katika doria
Polisi Haiti wakiwa katika doria dhidi ya magenge ya uhalifu.Picha: Odelyn Joseph/AP Photo/picture alliance

Msemaji wa wizara ya Usalama wa mambo ya ndani Marekani amesema, sera ya taifa lake haiwaruhusu watu ambao si raia na wasio na msingi wa kisheria kusalia nchini humo.

Afisa wa masuala ya uhamiaji nchini Haiti ameliambia shirika la habari la AFP kwamba jumla ya raia 52 wa Haiti waliwasili katika uwanja wa ndege wa mji wa Cap-Haitien hapo jana Alhamisi. 

Soma pia:Mamia ya mashirika yaiomba Marekani kutowarejesha raia wa Haiti wanaokimbia machafuko

Tangu mwishoni mwa mwezi wa Februari, magenge ya uhalifu yenye nguvu yameungana kuanzisha mashambulizi kote nchini nzima, ikiwemo vituo vya polisi, magereza na kusababisha kujiuzulu kwa waziri mkuu Ariel Henry.

Kutokana na mzozo huo unaozidi kuwa mbaya, karibu mashirika 500 ya kutetea haki za binadamu mwezi uliopita yaliandika barua iliyotumwa kwa maafisa wa Marekani akiwemo Rais Joe Biden, wakiomba kusitishwa kurudishwa kwa wahamiaji kutoka Haiti.