Korea Kaskazini yafanya jaribio la kombora
5 Julai 2017Msemaji wa wizara ya ulinzi ya Marekani amesema nchi yake imethibitisha kwamba Korea Kaskazini imefanya jaribio la kombora la IBM hapo jana Jumanne ambapo baadhi ya wataalamu hivi sasa wanaamini lina uwezo wa kufika umbali wa masafa ya jimbo la Alaska hali kadhalika maeneo mengine ya Marekani.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Rex Tillerson, amesema jaribio hilo lililofanyika katika mkesha wa siku ya mapumziko ya Siku ya Uhuru ya Marekani linawakilisha kupamba moto upya kwa tishio hilo dhidi ya Marekani na washirika wake na ameapa kuchukuwa hatua kali zaidi kukabiliana nalo.
Kwa mujibu wa shirika la haabri la serikali ya Korea Kaskazini, KCNA, kiongozi wa nchi hiyo, Kim Jong Un, amesema jaribio hilo limekamilisha uwezo wa nchi hiyo wa kumiliki silaha za kimkakati ikiwa ni pamoja na mabomu ya hydrogen na ICBM yenye wezo wa kurushwa na kufika mabara mengine.
Sharti la Korea Kaskazini kuzungumza na Marekani
Shirika hilo limemkariri Kim akisema serikali ya Korea Kaskazini haitozungumza na Marekani ili kuachana na silaha hizo hadi hapo serikali ya nchi hiyo itapoachana na sera zake za uhasimu dhidi ya nchi hiyo.
Akiwa na tabasamu pana usoni mwake, Kim amewaambia maafisa wa serikali, wanasayansi na mafundi kwamba Marekani haitofurahishwa kwa kuwa imepewa kifurushi cha zawadi wakati wa siku ya uhuru.
Taarifa ya shirika hilo imeongeza kusema kwamba Kim amewaamuru mara kwa mara kuendelea kuwapelekea vifurishi hivyo vikubwa na vidogo Wamarekani aliyowaita Mayankees.
Baraza la usalama kujadili hali hiyo
Waziri wa Masuala ya Kuiunganisha Upya Korea wa Korea Kusini amesema nchi hiyo bado inataka ufumbuzi wa amani katika eneo hilo la Korea.
Lakini mazoezi hayo ya kufyetuwa makombora pia yanaonekana kutuma ujumbe kwamba majirani wa nchi hiyo ya Korea Kaskazini wanaweza kutumia nguvu iwapo ikibidi. Cho Cha Mkuu wa majeshi wa Korea Kusini Chu Cha Gyu amesema "Iwapo Korea Kaskazini itaendelea kupuuza onyo letu la kijeshi na kuendelea na uchokozi tunaionya wazi kwamba utawala wa Kim Jon Un utakabiliwa na maagamizi."
Marekani imeliomba Baraza la Usalama la Umoja wa Matifa Jumatano (05.07.2017) kuitisha kikao cha dharura kujadili hali hiyo.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Rex Tillerson, amesema wanakusudia kuvifikisha vitendo hivyo vya uchokozi vya Korea Kaskazini kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na kuidhinishwa kwa hatua kali za kuiwajibisha serikali ya nchi hiyo.
Ameongeza kusema kwamba inachotaka Marekani ni kuziondowa kwa amani silaha za nyuklia katika rasi ya Korea na kukomesha vitisho vya Korea Kakazini.
Mwandishi: Mohamed Dahman/Reuters
Mhariri: Mohammed Khelef