1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yatarajiwa kutangaza vikwazo dhidi ya Urusi

Admin.WagnerD29 Desemba 2016

Miongoni mwa hatua ambazo zimejadiliwa ni pamoja na vikwazo vinavyolenga uchumi, kufungua mashtaka au kuvujisha taarifa zaidi kuiaibisha Urusi, na vikwazo dhidi ya wanadiplomasia wa Urusi.

https://p.dw.com/p/2V1CX
Mexiko G20 Gipfel Wladimir Putin und Barack Obama
Picha: Getty Images/AFP/J. Samad

 

Utawala wa Rais Barack Obama unatarajiwa kutangaza mikakati kadhaa ya vikwazo dhidi ya Urusi kwa kudukua data za asasi za kisiasa nchini Marekani, pamoja na data za watu binafsi kisha kuziweka wazi taarifa hizo, kwa lengo la kumsaidia rais mteule Donald Trump na Warepublican wengine. Wakati huo huo asasi moja ya kiusalama ya barani Ulaya imedai Urusi imekuwa ikijaribu kudukua data zake.

Maafisa wawili katika serikali ya Rais Obama ndio wamesema hayo bila kutaka kutajwa majina. Hata hivyo wote walikataa kufafanua ni hatua zipi rais ameidhinisha. Lakini wamesema miongoni mwa hatua ambazo zimejadiliwa ni pamoja na vikwazo vinavyolenga uchumi, kufungua mashtaka au kuvujisha taarifa zaidi kuiaibisha Urusi, na vikwazo dhidi ya wanadiplomasia wa Urusi.

Wamesema mojawapo ya uamuzi ambao umetolewa ni kuepuka hatua yoyote itakayozidi udukuzi huo wa kabla ya uchaguzi ili kuepuka kueneza mgogoro wa udukuzi mtandaoni jambo ambalo linaweza kutodhibitika. Mfano wa hatua ya kupindukia ni kuvuruga mfumo wa Urusi wa kutuma ujumbe kwa njia ya intaneti.

Mapema mwezi huu, Rais Obama alisema Marekani inahitaji kuchukua hatua na bila shaka itachukua hatua dhidi ya Urusi kwa kuingilia uchaguzi wa Marekani. Akirejelea suala hilo, Donald Trump amesema hajazungumza na maseneta wanaotaka Urusi kuwekewa vikwazo lakini atazungumza nao siku za baadaye.''Ninafikiria tunapaswa kuendelea na maisha yetu. Ninafikiri tarakilishi zina utata zaidi. Karne hii ya kompyuta imefanya hakuna anayejua haswa nini kinaendelea. Tunayo mengi ya kufanya lakini sina uhakika ikiwa tunao usalama tunaohitaji.'' Amesema Trump.

Maria Zakharova, Waziri wa Mambo ya Nje Urusi
Maria Zakharova, Waziri wa Mambo ya Nje UrusiPicha: picture-alliance/dpa/D. Serebryakov

OSCE yadai kundi la Urusi limejaribu kudukua data za bara la Ulaya

Wizara ya mambo ya nje ya Urusi imesema ikiwa Marekani itaiwekea Urusi vikwazo vipya kwa sababu ya madai ya udukuzi, basi itakuwa jaribio la kuvuruga uwezekano wa ushirikiano kati ya nchi hizo mbili. Shirika la habari la RIA limeripoti.

RIA limeinukuu wizara hiyo ambayo pia imesema inayo matumaini kuwa huenda rais mteule Donald Trump atavibatilisha vikwazo hivyo punde achukuapo hatamu za uongozi baada ya Rais Obama kuondoka mamlakani.

Wakati huo huo shirika la Usalama na Ushirikiano barani Ulaya OSCE, limekuwa likilengwa katika udukuzi. Msemaji wa shirika hilo amesema waligundua jaribio hilo mapema mwezi Novemba. Likinukuu duru kutoka kwa afisa wa ujasusi wa kimagharibi, gazeti la Ufaransa Le Monde limeripoti kuwa majaribio ya udukuzi huo yamefanywa na kundi kutoka Urusi lijulikanalo kama APT28. Kundi ambalo linadaiwa kuhusika katika udukuzi wa chama cha Democratic nchini Marekani.

Mwandishi: John Juma/RTRE

Mhariri: Grace Patricia Kabogo