Marekani yatangaza msaada wa kijeshi kwa Taiwan
29 Julai 2023Marekani imetangaza msaada wa kijeshi wa Dola milioni 345 kwa Taiwan, katika hatua inayoweza kuikasirisha zaidi China, katika wakati ambao uhusiano wa mataifa hayo mawili umezidi kudorora.
China, inayozidi kujiimarisha kidiplomasia na kijeshi, inadai kwamba kisiwa cha Taiwan kinachojitawala kidemokrasia, ni sehemu yake na imeapa kukitwaa kwa nguvu ikibidi.
Mvutano umeongezeka huku China ikifanya mazoezi ya mara kwa mara ya ndege za kivita na meli kuzunguka kisiwa hicho, huku Marekani ikionekana kujaribu kuipatia nguvu za kijeshi Taiwan ili kuzuia uvamizi unaoweza kujitokeza.
Afisa mmoja wa Marekani aliyezungumza kwa sharti la kutotajwa jina alidokeza siku ya Ijumaa kwamba, msaada huo utajumuisha vifaa vya kijasusi, uchunguzi na upelelezi sambamba na silaha ndogondogo. Bunge la Marekani liliidhinisha Rais Joe Biden kutoa msaada kijeshi kwa Taiwankama ilivyokuwa kwa Ukraine.