1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yasema Urusi inahusika na sumu dhidi ya Scripal

Isaac Gamba
15 Machi 2018

Balozi wa Marekani kwenye Umoja wa Mataifa Nikki Haley amelieleza Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuwa Marekani inaamini Urusi inapaswa kulaumiwa kwa shambulizi la sumu dhidi ya Scripal.

https://p.dw.com/p/2uMSE
USA UN Sicherheitsrat
Picha: picture-alliance/Photoshot

Jasusi huyo pamoja na mwanaye wako hospitali na hali zao ni mbaya kiafya baada ya kupewa sumu mjini Salisbury nchini Uingereza katika kile ambacho maafisa wa Uingereza wanasema ni sumu iliyotengenezwa Urusi.

Rais wa Marekani Donald Trump ameahidi kuiunga mkono Uingereza na kutoa mwito kwa Urusi kutoa ushirikiano. Hata hivyo balozi wa Urusi kwenye Umoja wa Mataifa Vassily Nebenzia amekanusha Urusi kuhusika na tukio hilo.

Nebenzia amesema  waziri mkuu wa Uingereza Theresa May anaonekana kutengeneza mazingira yasiyo ya kawaida wakati aliposema  kuna uwezekano mkubwa  Urusi inahusika kwa njia moja ama nyingine na kuhitaji maelezo zaidi  kutoka Urusi  ni kwa jinsi gani sumu hiyo ilitumika nchini Uingereza.

" Hatuzungumzi lugha ya kupeana muda hapa" alisema Nebenzia na kutoa mwito kwa Uingereza kukabidhi sampuli ya  sumu hiyo kwa ajili ya uchunguzi zaidi pamoja na  kutoa ushahidi unaothibitisha madai yao ya kuihusisha Urusi na tukio hilo.

Wakati wa kikao cha dharura kilichofanyika jana Jumatano, Haley alitoa mwito kwa Umoja wa Mataifa kuiwajibisha Urusi ambayo ni mwanachama wa kudumu wa baraza hilo la usalama la Umoja wa Mataifa kwa matendo yake. 

Naye naibu balozi wa Uingereza katika Umoja wa Mataifa Jonathan Allen alitoa mwito kuomba ushirikiano kutoka nchi wanachama wa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa na kuongeza kuwa hakuna hitimisho mbadala zaidi ya kusema Urusi inahusika na jaribio la kumuua Skripal pamoja na binti yake.

Großbritannien Theresa May, Premierministerin
Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa MayPicha: Reuters/Parliament TV

Ama kwa upande mwingine waziri wa mambo ya nje wa Uingereza Boris Johnson amesema hii leo kuwa kitu ambacho watu wanataka  ni kushuhudia vyombo vya kisheria vinawafikisha katika  mikono ya kisheria  matajiri wakubwa wanaoshirikiana na Urusi na ambao utajiri wao unaweza kuhusishwa na uhusiano wao na rais wa Urusi Vladimir Putin.

Hayo yanajiri mnamo wakati Uingereza ikiwafukuza wanadiplomasia 23 wa Urusi kufuatia tuhuma hizo za sumu iliyomdhuru jasusi wazamani ikiwa ni pamoja na kusimamisha mawasialiano ya ngazi ya juu yakiwemo yanayohusiana na fainali zijazo za kombe la dunia.

Ufaransa imesema inakubaliana na mtizamo wa Uingereza kuwa Urusi ndiyo imehusika katika kisa hicho cha Skripal kupewa sumu. Taarifa kutoka ofisi ya Rais Emmanuel Macron imesema tangu mwanzoni mwa wiki, Uingereza imekuwa ikiifahamisha Ufaransa kuhusu ushahidi uliokusanywa na unaoonyesha Urusi ilihusika.

Kwa upande wake wizara ya mambo ya nje ya Urusi imesema bado inafanyia kazi  hatua zilizochukuliwa na Uingereza dhidi ya Urusi kuhusiana na madai hayo ya kupewa sumu jasusi wa zamani  Sergei Skripal na kuhoji ni jinsi gani nchi nyingine zinaweza kuonyesha mshikamano na Uingereza katika sakata hili wakati hazina ushahidi.

Mwandishi: Isaac Gamba/dw/rtre

Mhariri :Caro Robi