1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yasitisha misaada ya kiusalama Pakistan

Caro Robi
5 Januari 2018

Misaada ya kiusalama kwa Pakistan yenye thamani ya takriban dola milioni 900 itasitishwa hadi Pakistan itakapochukua hatua madhubuti kupambana na kundi la wanamgambo wa Afghanistan la Taliban na la Haqqani.

https://p.dw.com/p/2qNGG
Pakistan Soldaten in Tatta Pani
Picha: picture-alliance/AP Photo/A. Naveed

Hatua hiyo iliyotangazwa na wizara ya mambo ya nje ya Marekani imesema inaonyesha kukerwa kwa utawala wa Rais Donald Trump kuwa Pakistan haijachukua hatua za kutosha dhidi ya makundi hayo mawili ambayo yamekuwa yakiitumia nchi hiyo kama sehemu ya kujificha na kufanya mashambulizi katika nchi jirani ya Afghanistan na kuwaua wanajeshi wa Marekani, wa Afghanistan na wa kutoka nchi nyingine.

Ufadhili huo utakaositishwa utaathiri ununuzi wa vifaa vya kijeshi, mafunzo, huduma nyingine za kijeshi na mpango wa kupambana na ugaidi. Akiwahutubia wanahabari, Msemaji wa wizara ya mambo ya nje wa Marekani Heather Nauert amesema hatua hiyo ya kusitisha ufadhili, haitaathiri misaada inayotolewa kwa raia wala zile za kusaidiai uchumi wa Pakistan

Miradi ya kijeshi itaathirika

Nauert amesema fedha hizo huenda zikadihinishwa kutolewa iwapo Pakistan itachukua hatua zinazostahili kukabiliana na makundi ya kigaidi, wakiongeza wanatumai Pakistan itaona hatua hiyo kama kupewa afueni na sio kupewa adhabu. Bunge la Marekani limefahamishwa kuhusu uamuzi huo wa kuistishia Pakistan misaada.

Pakistan kwa muda mrefu imekanusha shutuma kuwa imeshindwa kupambanana na makundi ya wanamgambo yanayopambana dhidii ya majeshi ya Afghanistan na ya kigeni kutokea upande wa pili wa mpaka.

Jalaluddin Haqqani
Kiongozi wa kundi la wanamgambo la Haqqani- Jalaluddin HaqqaniPicha: AP

Uhusiano kati ya Pakistan na Marekani umekuwa tete tangu tarehe mosi mwezi huu wakati Rais Donald Trump alipoishutumu nchi hiyo kupitia ukurasa wa Twitter kuwa licha ya kupewa misaada ya takriban dola bilioni 33, katika kipindi cha miaka 15 iliyopita inafanya kile alichokitaja danganya toto kwa kujifanya kupambana na ugaidi na wakati huo huo, kuwaruhusu wanamgambo wa Taliban na Haqqani wanaosakwa na Marekani kuitumia nchi hiyo kama ngome yake na hivyo kuwafanya viongozi wa Marekani kuonekana wapumbavu.

Pakistan imezitaja shutuma hizo za Trump kama zisizoelewa kabisa na zinazokinzana na kauli za waziri wa mambo ya nje Rex Tillerson na wa ulinzi James Mattis waliofanya ziara hivi karibuni Islamabad kwa kile kinachotajwa kujenga uaminifu kati ya Marekani na Pakistan.

Pakistan imeishutumu Marekani kwa kuitumia kama kisingizio kwa kushindwa kuleta amani nchini Afghanistan. Siku ya Alhamisi wiki hii, wizara ya mambo ya nje ya Marekani pia iliishutumu Pakistan kwa ukiukaji mkubwa wa uhuru wa kidini na kutangaza inaiweka nchi hiyo katika orodha ya nchi zinazofuatiliwa kwa undani.

Mwandishi: Caro Robi/Reuters/AP

Mhariri: Grace Patricia Kabogo