Janga
Marekani yashtushwa na wizi wa chakula Ethiopia
29 Juni 2023Matangazo
Shirika la misaada la Marekani USAID limeliambia shirika la habari la Associated Press haliridhirishwi na hali ya Ethiopia ambako maafisa wameripoti kutokea vifo kutokana na njaa katika wiki chache zilizopita baada ya Marekani na Umoja wa Mataifa kusitisha msaada wa chakula kutokana na wizi.
Maafisa wa Marekani wameshasema kibinafsi kwamba huu huenda ukawa wizi mkubwa kabisa wa chakula cha msaada kuwahi kutokea katika nchi yoyote duniani.
Marekani na Umoja wa Mataifa bado hawajasema ni nani aliyehusika na wizi huo uliogunduliwa kwa mara ya kwanza mwezi Machi katika eneo la kaskazini la Tigray, wakati tani za vyakula vya msaada kwa ajili ya watu wenye mahitaji zilipopatikana zikiuzwa kwenye magunia yaliyokuwa na alama ya bendera ya Marekani.