1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yashambulia mtandao wa al-Shabaab

2 Septemba 2014

Jeshi la Marekani limeushambulia mtandao wa kundi lenye itikadi kali za Kiislamu al Shabaab katika operesheni yake (01.09.2014) nchini Somalia. Shambilo hilo linatajwa kumlenga kiongozi anayejificha wa kundi hilo.

https://p.dw.com/p/1D5Eg
somalia milizen al-shabaab, al-shabab mogadischu
Wapiganaji wa al Shabaab wakiwa katika mazoezi ya kivita SomaliaPicha: AP

Kwa mujibu wa taarifa ya wizara ya ulinzi wa Marekani, Pentagon, shambulizi hilo lilikuwa likimlenga kiongozi aliyekuwa mafichoni wa mtandao huo. Msemaji wa Pentagon, John Kirb, amesema Marekani inafuatilia matokeo yake na itatoa maelezo zaidi pale taarifa itakapopatikana. Hata hivyo hakukuwa na taarifa zaidi zilizoweza kupatikana.

Afisa mwandamizi wa usalama nchini Somalia alisema ndege inayoruka bila ya rubani ilimlenga kiongozi wa al-Shabaab Ahmed Abdi Godane, muda mfupi baada ya kuondoka katika mkutano wa viongozi wa mtandao huo. Godane ambaye anajulikana pia kama Mukhtar Abu Zubeyr ni kiongozi wa kidini wa kundi hilo lenye mafungamano na mtandao wa kigaidi wa al-Qaeda.

Tetesi za kuuwawa Godane

Afisa mmoja wa Somalia aliyeongea pasipo kutaja jina lake kutokana na kutokuwa na mamlaka ya kufanya hivyo, amesema taarifa za uchunguzi zinaonesha anaweza kuwa ameuwawa sambamba na wapiganaji wengine. Taarifa zinaeleza kuwa shambulizi hilo limefanyika katika msitu mmoja ulio karibu na wilaya ya Sablale, umbali wa kilometa 170, kusini mwa Mogadishu, eneo ambalo al-Shabaab inalitumia kutoa mafunzo kwa wapiganaji wake.

Bildergalerie Somalia Sicherheitslage Shebab Anschlag 2013
Moja ya shambilizi la al ShebaabPicha: Mohamed Abdiwahab/AFP/Getty Images

Gavana wa jimbo la Lower Shabelle nchini Somalia, Abdiqadir Mohammed Nor, aliliambia shirika la habari la AP kwamba majeshi ya serikali na Umoja wa Afrika wanaelekea mji wa Sablale na kwamba walisikia mzizimo kama wa tetemeko la ardhi wakati ndege zinazoruka bila rubani zilipoishambulia kambi ya al Shabaab.

Mlolongo wa mashambulizi ya Marekani nchini Somalia

Marekani imekuwa ikifanya mashambulizi ya angani nchini Somalia katika miaka ya hivi karibuni. Shambulizi lake la kombora lake la mwezi Januari liliweza kumua afisia wa ngazi wa juu kabisa katika masuala ya usalama wa al Shabaab na mwezi wa kumi mwaka uliyopita gari iliyokuwa imebeba wanachama wa kundi hilo ilishambuliwa na kusababisha kifo cha mtaalamu wa juu kabisa wa viripuzi wa mtandao huo.

Hatua hii ya sasa ya Marekani kinatokea baada ya majeshi ya serikali ya Somalia kufanikiwa kulirejesha katika udhibiti wake gereza kubwa mjini Mogadishu, ambalo lilishambuliwa na watu saba wenye silaha nzito, ambao wanahisiwa kuwa wanamgambo, walikuwa katika jaribio la kutaka kuwaachia huru wenzao wengine wenye itikadi kali ambao wamefungwa. Hata hivyo taarifa ya Pentagon haijaeleza kama shambulizi hili linahusiana na lile la gerzani au la.

Maafisa nchini Somalia wanasema washambuliaji wote sana, wanajeshi watatu wa serikali na raia wawili waliuwawa. Gereza la Godka Jilacow la mijini Mogadishu ni kituo mahojiano cha idara ya upelezi ya Somalia ambapo kunaelezwa kuwepo kwa wafungwa kutoka kundi la al-Shabaab ambao wanashikiliwa chini ya ardhi.

Mwandishi: Sudi Mnette APE
Mhariri: Josephat Charo