1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yasema Urusi inapanga kufanya mashambulizi Kyiv

Babu Abdalla23 Agosti 2022

Marekani imesema Urusi inapanga kuongeza mashambulizi nchini Ukraine wakati nchi hiyo inajiandaa kuadhimisha miaka 31 ya uhuru wake kutoka utawala wa Kisovieti kesho Jumatano.

https://p.dw.com/p/4FuV3
Ukraine | Zerstörte russische Panzer
Picha: Sergei Chuzavkov/SOPA Images via ZUMA Press/picture alliance

Mkurugenzi katika ofisi ya rais wa Poland Andrzej Duda, Pawel Szrot, amewaambia waandishi wa habari kuwa ziara ya Duda itajumuisha mkutano na rais Volodymyr Zelenskiy, na pia mazungumzo juu ya msaada wa kijeshi, kiuchumi, masuala ya kibinadamu na kisiasa pamoja na mambo mengine.

Bwana Szrot ameeleza kuwa viongozi hao wawili watajadili kuhusu jinsi Poland inavyoweza kuzishawishi nchi nyengine kuendelea kuipa msaada zaidi Ukraine.

Soma pia: Urusi: Ukraine inahusika na kifo cha binti wa mshirika wa Putin

Tayari, Duda amekutana na Zelenkskiy mara tano mwaka huu, ikiwa ni pamoja na ziara tatu alizozifanya ndani ya Ukraine tangu kuanza kwa uvamizi huo, ambao Urusi unaita "oparesheni maalum ya kijeshi."

Poland ni moja kati ya nchi zinazoiunga mkono kwa dhati Ukraine na karibu wakimbizi milioni sita wa Ukraine wamevuka mpaka na kuingia nchini Poland tangu Urusi ilipoivamia nchi hiyo Februari 24.

Licha ya kuwapa hifadhi mamilioni ya wakimbizi wa Ukraine, Poland ambayo ni nchi mwanachama wa jumuiya ya kujihami ya NATO na Umoja wa Ulaya, imekosolewa na baadhi ya mataifa mengine ya Umoja huo kwa kutofanya zaidi kuisaidia Ukraine.

Rais wa Poland amewasili Kyiv kujadili juu ya kupeleka msaada zaidi kwa Ukraine

Ukraine Krieg Andrzej Duda in Kiew
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy(kulia) na Rais wa Poland Andrzej Duda kabla ya mkutano waoPicha: Ukrainian Presidential Press Service/Reuters

Ubalozi wa Marekani mjini Kyiv umeonya juu ya uwezekano wa kuongezeka kwa mashambulizi ya kijeshi ya Urusi nchini Ukraine katika siku zijazo karibu na siku ya kuadhimisha uhuru wa Ukraine. Ubalozi huo umewataka raia wa Marekani kuondoka nchini humo iwapo watapata nafasi ya kufanya hivyo.

Soma pia: Zaporizhhzhia: Ukraine na Urusi zatupiana lawama:

Rais Volodymyr Zelenskiy ametahadharisha kile alichokiita kuwa Urusi inaweza "kujaribu kufanya kitu cha kutisha” kuelekea maadhimisho ya siku ya uhuru, ambayo pia yanakwenda sambamba na miezi sita kamili tangu Urusi ilipoivamia Ukraine.

"Hatutawahi kutambua rangi za nchi nyingine kwenye ardhi na anga yetu. Daima tuko tayari kutetea bendera yetu yenye rangi za samawati na njano. Ninawaomba nyote kuwakumbuka mashujaa waliojitolea maisha yao kwa ajili kuitetea nchi yetu," amesema Zelenskiy.

Ubalozi wa Marekani kupitia tovuti yake imeandika kuwa, wizara ya mambo ya nje ya nchi hiyo imepata habari kuwa Urusi inapanga kuongeza mashambulizi yake dhidi ya raia wa Ukraine, miundo mbinu na taasisi za serikali katika siku chache zijazo.

Mamlaka nchini Ukraine imepiga marufuku sherehe za umma katika mji mkuu wa Kyiv wakati wa maadhimisho ya miaka 31 ya uhuru wa Ukraine kutoka utawala wa Kisovieti kesho Jumatano, ikitoa sababu za kuwepo kwa tishio kubwa la usalama.