1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yaruhusu ujenzi wa bomba la mafuta la XL

24 Machi 2017

Serikali ya Marekani imetoa kibali cha rais kwa ajili ya kuendelea na mradi wa ujenzi wa bomba la mafuta la Keystone XL kutoka Canada kwenda Marekani.

https://p.dw.com/p/2ZuRn
Keystone Pipeline TransCanada Pumpstation
Picha: picture-alliance/AP Photo/N. Harnik

Mradi uliokuwa na utata kuhusu ujenzi wa bomba la mafuta ghafi kutoka Canada kwenda Marekani ulizuiwa na Rais wa zamani wa Marekani, Barack Obama kutokana na wasiwasi wa uharibifu wa kimazingira.

Wizara ya mambo ya nje ya Marekani imesema kibali hicho kimesainiwa leo na Naibu Waziri wa Wizara ya Mambo ya Nje anayehusika na Masuala ya Kisiasa, Thomas Shannon Jr, ambaye amehitimisha uamuzi ambao unaonekana kama ''utatumika kwa maslahi ya taifa.''

Rais wa Marekani, Donald Trump alitoa ruhusa ya kuendelezwa kwa mradi huo utakaogahrimu Euro bilioni 7.4, mwezi Januari wakati alipochukua hatua wakati wa siku zake za kwanza madarakani.

Serikali ya Obama iliusimamisha mredi huo mwaka 2015, baada ya miaka kadhaa ya kuutathmini, huku ikielezea wasiwasi wa kimazingira.

Ahadi ya Trump

Hata hivyo, wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa urais, Trump aliahidi kuidhinisha ujenzi wa mradi huo, akisema utasaidia kuanzisha maelfu ya ajira na kuimarisha sekta ya mafuta.

TransCanada Keystone Pipeline
Pichani ni mmoja wa wanamazingira wanaopinga mradi huoPicha: picture alliance/empics/The canadian Press/D. Dyck

Kwa mujibu wa Wiraza ya mambo ya nje, ruhusa hiyo imetolewa baada ya kufanya tathmini mpya kuhusu mradi huo na kuzingatia maslahi na athari za kiuchumi, sera ya kigeni pamoja na nishati.

Kampuni ya mafuta na nishati ya TransCanada ambayo awali iliomba kibali cha kujenga bomba hilo mwaka 2008, limeuita uamuzi huo kama ''hatua muhimu.''

Pindi mradi huo utakapokamilika, bomba hilo litakalokuwa na urefu wa kilomita 1,900, litasafirisha mapipa 800,000 ya mafuta kwa siku kutoka Alberta, Canada kwenda kwenda kampuni za kusafisha mafuta ghafi katika pwani ya Ghuba ya Texas.

Uamuzi huo ni pigo kubwa kwa wanamazingira na wanaharakati wa Kimarekani ambao wamesema mradi wa ujenzi wa bomba hilo utaharibu ardhi inayotumika kwa ajili ya mazishi, kuhatarisha vyanzo vya maji na kuchangia katika uchimbaji unaohusiana na ongezeko la joto duniani.

Watu wa Standing Rock Sioux na makabila mengine wamekuwa wakiandamana kwa miezi kadhaa sambamba na makundi yenye kulinda mazingira kuhusu ujenzi wa bomba hilo pamoja na thari zake.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/Reuters, AFP, AP, DPA
Mhariri: Iddi Ssessanga