1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yaridhia Israel iuzie Ujerumani mfumo wa Arrow 3

17 Agosti 2023

Israel imesema Marekani imeridhia mauzo ya kihistoria ya mfumo wa kisasa wa ulinzi wa anga aina ya Arrow 3 kwa Ujerumani. Makubaliano hayo yenye thamani ya dola bilioni 3.5, ni makubwa zaidi ya kijeshi katika nchi hiyo.

https://p.dw.com/p/4VHlx
Israel Arrow Raketensystem/Hatzor Luftstützpunkt
Picha: ZUMA/IMAGO

Israel imesema Marekani imeridhia mauzo ya kihistoria ya mfumo wa kisasa wa ulinzi wa anga aina ya Arrow 3 kwa Ujerumani. Makubaliano hayo yenye thamani ya dola bilioni 3.5, ni makubwa zaidi ya kijeshi katika nchi hiyo.

Mfumo wa ulinzi wa makombora chapa Arrow 3, ambao umetengenezwa na Israel kwa ushirikiano na Marekaniumeundwa kwa lengo la kudungua makombora ya masafa marefu juu ya angahewa.

Wizara ya Ulinzi ya Israel imesema kupitia taarifa kwamba wizara ya mambo ya nje ya Marekani imeiarifu kuhusu idhini ya serikali ya Marekani kwamba inaweza kuiuzia Ujerumani mfumo huo wa Arrow 3.

Ridhaa ya Marekani inazingatiwa kuwa hatua ya kuondolewa kikwazo cha mwisho katika njia ya kufikia mapatano juu ya masuala ya ulinzi baina ya Israel na Ujerumani.

"Wizara ya Ulinzi ya Israel, Wizara ya Shirikisho la Jeshi la Ujerumani na kampuni ya Aerospace ya Israel, wamesaini makubaliano hayo ya kihistoria yenye thamani ya dola 3.5 ya ulinzi,” taarifa hiyo imesema.

Soma pia:Antony Blinken amewasili mjini Jerusalem kukamilisha

Wizara hiyo imesema maafisa wa ngazi ya juu kutoka wizara za ulinzi za Ujerumani na Israelzitatia saini ahadi ya kujitolea kuyaheshimu makubaliano hayo na kutoa malipo ya awali ya dola milioni 600.

Taarifa hiyo imeendelea kusema "kutokana na uwezo wake wa kipekee wa kuzuia makombora ya masafa marefu yanayopaa juu zaidi angani, mfumo wa Arrow 3 ni mfumo wa ulinzi wa aina yake.”

Gallant: Makubaliano haya ni ya kihistoria

Ripoti hiyo ilimnukuu waziri wa Ulinzi wa israel Yoav Gallant akiyataja makubaliano hayo kuwa "makubwa zaidi katika historia ya Israel”.

"Huu ni uamuzi muhimu utakaochangia katika kujenga nguvu na uchumi wa Israel,” alisema.

Israel Politik Yoav Gallant
Waziri wa Ulinzi Israel Yoav GallantPicha: Maya Alleruzzo/AP/picture alliance

Mkurugenzi mtendaji wa shirika la Ulinzi la Makombora la Israel Moshe Patel, amesema wanazungumza na Ujerumanikuhusu mfumo wa ulinzi, ambapo Israel inaenda kuwalinda raia wa Ujerumani, miaka 78 tangu mauaji ya halaiki dhidi ya Wayahudi, Holocaust.

Mfumo wa Arrow ambao unafadhiliwa kwa kiasi na Marekani, ulitengenezwa na kampuni ya Aerospace ya Israel (IAI) kwa ushirikiano na Boeing.

Soma pia:Biden, Herzog wazungumzia mivutano ya Israel katika ikulu ya White House

Kulingana na viwanda hivyo, mfumo wa Arrow 3 unaweza kuzuia makombora ya masafa marefu umbali wa kilomita 2,400.

Mfumo huo unatarajiwa kuanza kutumika kwa ajili ya ulinzi wa Ulayakuanzia miaka miwili ijayo.

Ili kufanikisha mradi huo, Patel amesema kampuni ya IAI itaweka miundombinu mipya kwa ajili ya Ujerumani na itawaajiri wahandisi wapya na wataalam wa Israel na Marekani kwa utengenezaji.

Amewaambia waandishi habari kwamba serikali ya Ujerumani inataka uwe sawa na mfumo wanaotumia.