Marekani yaruhusu kampuni za nje kushirikiana na Iran
31 Machi 2020Waziri wa Nje wa Marekani Mike Pompeo ameidhinisha hatua hiyo ingawa ameonya kuwa kamwe hakubaliani na kile alichokiita mipango ya silaha za nyuklia ya Iran.
Duru kutoka ndani ya utawala wa Rais Trump zinasema kuwa waziri huyo wa mambo ya kigeni alikuwa akipingana na uamuzi huo lakini Waziri wa Fedha Steven Mnuchin alishikilia kwamba katika wakati ambao Iran inakabiliwa na janga la kirusi cha corona hiyo ilikuwa hatua pekee ya kibinaadamu inayofaa kuchukuliwa.
"Kama alivyosema Rais Trump mapema mwaka huu, Iran haitaruhusiwa kamwe kuwa na silaha ya nyuklia. Tutaendelea kufuatulia kwa karibu mwendelezo wa programu ya nyuklia ya Iran na tunaweza kubadilisha vikwazo hivi muda wowote." Alisema msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje, Morgan Orgatus, akiongeza kuwa "vikwazo hivyo vimeondoshwa kwa siku 60 zaidi."
Uamuzi huo wa kuondowa vikwazo kwa kampuni zisizo za Kimarekani unazipa nafasi ya kufanya kazi na shirika la nishati ya atomiki la Iran.
Vikwazo vipya vyaimarishwa
Hatua hiyo ya utawala wa Trump, ambao mwaka 2018 ulijiondowa kwenye makubaliano ya mwaka 2015 juu ya mpango wa nyuklia wa Iran na kurejesha upya vikwazo kwa Iran, utaruhusu kazi zisizohusiana na silaha za nyuklia kuendelea kwenye vinu vya nyuklia vya Arakm, Busher na Tehran, pamoja na shughuli nyenginezo za nyuklia.
Kama sehemu ya kampeni yake ya kuibinya Iran, Marekani sio tu imerejesha vikwazo vya awali ilivyoviondowa baada ya mkataba wa mwaka 2015, bali pia imeongeza na vyengine vipya kwa madai ya kuizuwia Iran isiendeleze uundaji wa makombora, silaha za nyuklia na kuacha uchokozi dhidi ya majirani zake.
Wiki iliyopita, serikali ya Marekani ilitangaza vikwazo vipya kwa maafisa 20 na kampuni za Iran kwa madai ya kuliunga mkono kundi la wanamgambo wa Kishia nchini Iraq lililohusika na mashambulizi dhidi ya vituo vyake vya kijeshi kwenye eneo hilo.
Sera ya Marekani kuhusu Iran imekuwa ikikosolewa vikali ndani na nje ya Iran, huku utawala mjini Tehran ukisema kwamba inakwamisha juhudi za taifa hilo la Ghuba kukabiliana na mripuko wa kirusi cha corona, ambao hadi sasa umeshaangamiza maisha ya Wairani 2,460 miongoni mwa takribani watu 40,000 waliokwishaambukizwa.