1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yapigia upatu mkataba wake na Taliban

6 Machi 2020

Marekani imeanza mashauriano na wajumbe wengine wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa lengo la kutayarishwa azimio litalounga mkono mkataba wa amani kati ya nchi hiyo na kundi la Taliban la nchini Afghanistan. 

https://p.dw.com/p/3YwvB
New York UN Sicherheitsrat Sondersitzung Syrien
Picha: picture-alliance/AA/T. Coskun

Kulingana na rasimu ya awali ya azimo hilo iliyopatikana na shirika la Habari la AFP, baraza la usalama la Umoja wa Mataifa limeukaribisha mkataba wa amani uliotiwa saini mjini Doha mnamo Februari 29.

Azimio hilo linatoa wito kwa mataifa yote hususani yaliyo kwenye kanda ya mataifa ya kiarabu kutoa uungaji mkono utakaowezesha kupatikana mpango mpana zaidi na wa kudumu wa amani kwa ajili ya Afghanistan.

Hata hivyo hadi sasa China na Urusi hazijaweka wazi misimamo yao kuhusu pendekezo la azimio hilo.

Rasimu hiyo ya Marekani pia italenga kutoa shinikizo kwa serikali ya Afghanistan kufanya mazungumzo na Taliban kufanikisha makubaliano ya kudumu ya kusitisha mapigano.

Mkataba utafungua njia ya amani 

Afghanistan Kabul | Jens Stoltenberg, NATO & Aschraf Ghani, Präsident & Mark Esper, USA
Picha: Getty Images/AFP/W. Kohsar

Chini ya mkataba wa Doha serikali ya Afghanistan inatakiwa kuwaachia huru wanamgambo 5,000 wa Taliban na kundi hilo litaawachia huru wafungwa 1000 wa upande wa serikali.

Mazungumzo kati ya serikali mjini Kabul na kundi la Taliban yaliayotajwa kwenye rasimu ya azimio la Marekani yanapaswa kuanza wiki ijayo mjini Oslo nchini Norway.

Katika azimio linalopigiwa upatu na Marekani, Washington imesema pindi mazungumzo hayo yataanza Baraza la usalama litapitia upya vikwazo vilivyowekwa dhidi ya watu au makundi ya wapiganaji tangu mwaka 2011 kwa lengo ya kulegeza au kuviondoa katika juhudi za kuchochea kupatakana amani.

Mkataba kati ya Marekani na Taliban pia utafungua njia kwa Marekani kuondoa wanajeshi wake kutoka Afghanistan baada ya zaidi ya miaka 18 ya vita kwa makubaliano kwamba kundi hilo lisitisha shughuli zote za kigaidi.

Machafuko bado yanayotokea Afghanistan 

Afghanistan Taliban Konflikt
Picha: Getty Images/N. Shirzada

Hata hivyo licha ya kufikiwa mkataba huo bado mapigano ya hapa na pale yameripotiwa nchini Afghanistan.

Mapema leo kumetokea shambulizi la roketi na mapambano ya kutumia bunduki katika mkutano wa kisiasa uliohudhuriwa na moja ya wanasiasa vigogo nchini humo Abdullah Abdullah lakini aliondolewa bila kupata madhara.

Wizara ya mambo ya ndani ya nchi imesema kikosi maalum cha polisi kimetumwa kwenye eneo hilo kwa uchunguzi.

Hakuna kundi lililodai kuhusika na shambulizi hilo.

Katika hatua nyingine mahakama ya kimataifa ya makosa ya uhalifu wa kivita ICC, imeidhinisha kufanyika uchunguzi kuhusu uwezekano wa kuwepo makosa ya kivita na uhalifu dhidi ya binadamu uliyofanywa nchini Afghanistan.

Maamuzi wa kuanzisha uchunguzi huo unaoilenga Marekani, Afghanistan pamoja na wanamgambo wa Taliban umekuja baada ya wajaji kukubali rufaa ya waendesha mashtaka dhidi ya uamuzi wa hapo kabla wa kuzuia kufanyika uchunguzi.

Mwaka uliopita majaji wa ICC walikiri kuwepo kwa uhalifu mkubwa nchini Afghnaistan lakini walikataa kufanyika uchunguzi kwa msingi kuwa muda mrefu umepita tangu kuanza kwa machafuko na wasiwasi wa kukosekana ushrikiano wa jumuiya ya kimataifa.