Marekani yaonya juu ya mashambulio mapya Nigeria
7 Novemba 2011Onyo hilo limekuja baada ya watu kiasi ya 150 kuuawa kufuatia mfululizo wa mashambulio yaliyofanywa na kundi la kiislamu lililo na msimamo mkali liitwalo Boko Haram kaskazini mashariki mwa taifa hilo.
Mashambulio ya Ijumaa iliyopita ndiyo yalikuwa mabaya zaidi kuwahi kufanywa na kundi hilo la kiislamu lililo na msimamo mkali, Boko Haram, lenye ngome yake kaskazini mwa taifa hilo lililo na idadi kubwa ya watu barani Afrika.
Ubalozi wa Marekani nchini Nigeria umeonya kuwa kundi hilo huenda likashambulia mahoteli na maeneo mengine katika mji mkuu, Abuja, wakati huu wa sherehe za Eid Al-Adhha.
Taarifa kutoka ubalozi huo ilisema baada ya Boko Haram kushambulia majimbo ya Borno na Yobe, wamepokea taarifa kuwa kundi hilo linapanga kushambulia maeneo kadhaa katika mji mkuu wa taifa hilo.
Usalama uliimarishwa mjini Abuja ambao umekuwa ukilengwa mara kadhaa, ikiwemo shambulio la kujitoa mhanga la tarehe 26 mwezi Agosti dhidi ya makao makuu ya umoja wa mataifa liliosababisha vifo vya watu 24.
Ubalozi wa Marekani ulisema maeneo yanayoweza kulengwa ni pamoja na hoteli za kifahari za Nicon Luxury, Sheraton na Transcorp Hilton, na kuwataka wafanyikazi wa ubalozi huo kuyaepuka maeneo hayo.
Afisa mmoja wa polisi alisema karibu polisi 1300 na kikosi maalum cha kukabiliana na ugaidi walitumwa katika makanisa, misikiti na maeneo mengine muhimu katika mji huo mkuu hapo jana. Waumini walifanyiwa upekuzi kwa vifaa vya kutambua silaha kabla ya kuingia makanisani na katika mji wa Damaturu ambapo watu 150 waliuwawa, maelfu ya waislamu walisali sala za Eid al Adha katika ukumbi ulio wazi uliokuwa umezingirwa na maafisa wa polisi.
Rais Jonathan Goodluck ambaye aliyataja mashambulio ya hivi karibuni katika jimbo la Yobe kuwa ya kuchukiza, aliwaomba waislamu wakati huu wanaposherehekea Eid kuiombea nchi hiyo amani.
Hapo awali, kundi hilo haramu lilikuwa likiyalenga makanisa, wanasiasa na maafisa wa usalama, lakini hivi karibuni wamekuwa wakiwafyatulia risasi kiholela watu katika mitaa, bila kujali wanatoka tabaka gani.
Msemaji wa idara ya kushughulikia mikasa ya dharura nchini Nigeria, Ibrahim Farinloye, alisema visa hivyo havichagui kabila, dini au taaluma, akisema hilo ndilo limesababisha idadi kubwa ya vifo .
Baba mtakatifu Benedict wa kumi na sita alitoa wito wa kukomeshwa machafuko hayo, akisema hayasuluhishi matatizo, bali yanayaongeza na kupanda mbegu ya chuki na migawanyiko.
Chama cha upinzani cha Action Congress kilisema kimeshtushwa na kiwango cha mashambulio na kuilaumu serikali kwa kushindwa kukabiliana na tatizo hilo.
Sani Shehu wa chama cha haki za kijamii nchini Nigeria alisema harakati za vikosi vya usalama vya serikali huenda vimechochea mashambulio hayo.
Boko Haram lilikiri kuhusika na mashambulio ya ijumaa na kuonya kuwa itafanya mashambulio zaidi. Kundi hilo haramu ambalo linataka kuunda jimbo la kiislamu kaskazini mwa Nigeria lijaribu kufanya maasi mwaka 2009 ambayo yalizimwa vikali na maafisa wa usalama.
Mwandishi: Caro Robi/AFP
Mhariri:Othman Miraji.