1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yamuwekea vikwazo mshauri wa Kabila

2 Juni 2017

Marekani imemuwekea vikwazo mshauri mkuu wa Rais Joseph Kabila wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na kuiongezea shinikizo serikali yake kuhusiana na kuchelewesha uchaguzi na madai ya ukiukaji wa haki za binaadamu.

https://p.dw.com/p/2e21s
Joseph Kabila
Rais wa DRC Joseph KabilaPicha: picture alliance/dpa/A.Gomber

Hatua hiyo inafuatia tangazo lililotolewa na Umoja wa Ulaya, hapo Jumatatu la kuwawekea vikwazo vya usafiri na kuwafungia mali zao raia 9 wa Congo, hiyo ikiwa ni njia mojawapo ya kuisukuma serikali ya Congo kuandaa uchaguzi kumchagua atakayeichukua nafasi ya Kabila kabla mwishoni mwa mwaka.

Mara kadhaa Congo imeshutumu vikwazo inavyowekeea na Umoja wa Ulaya na Marekani kama visivyo vya haki na kinyume cha sheria, na imetishia kujibu kidiplomasia.

Idara ya fedha ya Marekani ilimuweka Jenerali Francois Olenga katika orodha maalum ya watu, na kuifungia mali yoyote aliyonayo Marekani na kuwazuia Wamarekani kujihusisha katika biashara ya aina yoyote naye. Haijabainika iwapo Olenga anamiliki mali zilizo chini ya himaya ya Marekani.

Marekani inatuma ujumbe mkali kwa jeshi la Congo

Katika taarifa yake, idara hiyo ilisema Olenga Olenga ambaye alipigana pamoja na baba yake Joseph Kabila, Laurent Kabila, katika vile vita vilivyomuondoa madarakani dikteta Mobutu Seseseko mwaka 1997, anasimamia kikosi cha walinzi ambacho kinawatisha wale wanaomkosoa Kabila na kuwakamata na hata kuwauwa raia wa Congo.

Rebellen eroberen Kinshasa - Mobutu auf der Flucht
Dikteta wa zamani wa Congo Mobutu Sese sekoPicha: picture-alliance/dpa/Feferberg

Mkurugenzi wa idara hiyo kitengo kinachodhibiti mali za nje ya nchi John E. Smith alisema, "hatua hii dhidi ya Olenga inaonesha ujumbe mkali tunaoutoa kwa jeshi la Congo kwamba kuendelea kwake kuwanyanyasa raia wake ni jambo ambalo halikubaliki."

Serikali ya Congo imekanusha kwamba inatumia nguvu kupita kiasi dhidi ya raia wake.

Idara hiyo ya fedha ya Marekani pia iliiwekea vikwazo hoteli moja iitwayo Safari Resort inayomilikiwa na Olenga na iliyoko viungani mwa mji mkuu wa Congo, Kinshasa. Olenga na msemaji wa jeshi la Congo hawakupatikana kwa wakati kujibu kuhusiana na vikwazo hivyo vipya. Waziri wa Habari wa Congo, Lambert Mende, aliyewekewa vikwazo wiki hii na Umoja wa Ulaya pia, alisema hafahamu kuhusiana na vikwazo hivyo dhidi ya Olenga.

Maafisa wa usalama waliuwawa waandamanaji wakati wa maandamano mwaka jana

Kabila aliye madarakani tangu mwaka 2001, alikataa kuondoka wakati muhula wake ulipomalizika mwezi Desemba. Chini ya mkataba ulioafikiwa pamoja na upinzani nchini humo, uchaguzi unastahili kuandaliwa kufikia mwishoni mwa mwaka huu, ingawa mchakato wa maandalizi umesita kutokana na ajizi ya kuwasajili wapiga kura.

Syrien Kinder im Krieg in Aleppo
Barack Obama aliwashutumu sana viongozi wa Afrika waliokatalia madarakani wakati wa utawala wakePicha: picture-alliance/AA/E. Sansar

Maafisa wa usalama waliwauwa watu kadhaa katika maandamano dhidi ya Kabila mwaka jana, na kuibua hofu kwamba nchi hiyo inaelekea kutumbukia tena katika mapigano ya wenyewe kwa wenyewe yaliyoshuhudiwa katika miaka ya nyuma ambapo mamilioni ya watu waliuwawa.

Mwaka jana Marekani iliwawekea vikwazo maafisa watano wa Congo kwa madai ya ukiukaji wa haki za binaadamu na miongoni mwa maafisa hao walikuwa ni mkuu wa taifa wa ujasusi na waziri wa usalama wa ndani wakati huo.

Marekani chini ya utawala wa Barack Obama ilikuwa inawashutumu sana viongozi wa Afrika wanaong'ang'ania madarakani, ingawa tangu Donald Trump aingie, nchi hiyo imekuwa kimya kuhusiana na masuala ya Afrika.

Mwandishi: Jacob Safari/Reuters/HRW

Mhariri: Mohammed Khelef