1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yamuua kamanda wa juu wa Iran

3 Januari 2020

Kamanda wa ngazi ya juu wa Iran Qasem Soleimani ameuawa katika shambulio la Marekani katika mji mkuu wa Iraq Baghdad, huku Iran ikiapa kulipiza kisasi, hali inayozidisha mzozo mbaya kati ya Tehran na Washington.

https://p.dw.com/p/3VfWa
Iran Kommandeur Al-Kuds-Brigaden General Ghassem Soleimani
Picha: Farsnews

Wizara ya ulinzi ya Marekani Pentagon imesema Rais Donald Trump aliamuru kuuawa kwa Soleimani baada ya kundi la waandamanaji wanaoiunga mkono Iran kuuzingira ubalozi wa Marekani. 

Kiongozi mkuu wa Iran Ayatollah Ali Khamenei ameapa kulipiza kisasi kifo cha Soleimani, katika ongezeko kubwa zaidi la vita vya uwakala kati ya Iran na Marekani katika ardhi ya Iraq.

Wakati Ubalozi wa Marekani ukiwahimiza raia wa Marekani kundoka mara moja nchini Iraq, Trump alitweet picha ya bendera ya Marekani bila kutoa maelezo yoyote.

Mapema Ijumaa, mkururo wa mashambulizi ya makombora yaliulenga uwanja wa ndege wa kimataifa wa Baghdad, na kuushambulia msafara wa magari wa Hashed al-Shaabi, ambalo ni kundi la kijeshi la Iraq lenye mafungano ya karibu na Iran.

Irak Bagdad Airport Luftschlag US-Streitkräfte auf General Qassem Soleimani
Picha hii inaonyesha gari lililoharibiwa likiwaka moto kufuatia shambulio la Marekani Januari 3, 2020 kwenye barabara ya uwanja wa kimataifa wa Baghdad, ambamo Jenerali Qasem Soleimani na naibu kamanda wa kundi la Hashedi al-Shaabi Abu Mahdi Al-Muhandis waliuawa.Picha: AFP/Iraqi Military

Saa chache baadae, Jeshi la Ulinzi wa Mapinduzi la Iran likatangaza kuwa Soleiman ameuawa shahidi na Marekani katika uwanja wa Baghdad asubuhi ya leo.

Kundi la Hashed likathibitisha kuwa Solaimani pamoja na naibu kamanda wake Abu Mahdi al-Muhandis wameuawa katika kile lilichokitaja kuwa shambulio la Marekani lililolenga gari lao kwenye barabara ya kuelekea uwanja wa ndege wa kimataifa wa Baghdad.

"Sisi, wanachama wa jeshi la ulinzi wa mapinduzi tumehuzunishwa sana na habari hizi, Hata hivyo, dhamira yetu ya kujibu mashambulizi dhidi ya uhalifu wa Marekani na wazayuni wakaliaji imeimarishwa na bila shaka hili litatokea," alisema msemaji wa kikosi cha ulinzi wa mapinduzi Jenerali Ramezan Sharif.

Mataifa yazungumzia mauaji hayo

Waziri mkuu wa Iraq anaeondoka Adel Abdul-Mahdi amelaani mashambulizi ya Marekani na kuitishia kikako cha dharura cha Bunge kuchukuwa kile alichokiita hatua stahiki zinazohitajika ili kulinda hadhi, mamlaka na uhuru wa Iraq.

Mataifa mengine pia yamezungumzia mauaji hayo ambapo Urusi imesema yanaweza kuchochea zaidi mzozo katika kanda ya Mashariki ya Kati, huku Ufaransa ikisema mauaji ya Soleimani hayatatuliza mzozo bali yatauchochea zaidi.

Iran Kommandeur Al-Kuds-Brigaden General Ghassem Soleimani
Jenerali Qasem Soleimani akiteta jambo na kiongozi mkuu wa Iran Ayatollah Ali Khamenei wakati wa uhai wake.Picha: ravapress.ir

China kwa upande wake imeomba pande zote kujizuwia huku utawala wa Syria ukilaani pia mauaji hayo uliyoyataja kama ya kiuoga kwa upande wa Marekani.

Nchini Marekani kwenye, wanasiasa wa juu wa chama cha Republican wamesifu hatua hiyo ya rais Trump mnamo wakati bunge likilalamika kutojulishwa mapema juu ya shambulio hilo.

Sifa kubwa kutoka wabunge wa Republican zimekuwa kinyume kabisaa na Wademokrat waliokosa vikali hatua hiyo ya Trump katika ishara ya mgawanyiko mjini Washington kueleka uchaguzi wa rais mwaka huu.

Na huko Israel, ofisi ya waziri mkuu Benjamin Netanyahu imesema waziri mkuu huyo amekatisha ziara yake nchini Ugiriki kufuatia mauaji hayo, na kituo cha redio ya jeshi kimeripoti kuwa jeshi limeogeza tahadhari kwa kuhofia ulipizaji kisasi wa Iran au mawakala wake katika kanda hiyo dhidi ya maslahi ya Israel.