1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaMarekani

Marekani yakataa kulitambua taifa la Palestina

19 Aprili 2024

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limekataa kuidhinisha azimio la kuipatia Palestina uwanachama kamili baada ya Marekani kutumia kura yake ya turufu kuzuia azimio hilo

https://p.dw.com/p/4exjs
Mkutano wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa mjini New York Marekani kupigia kura azimio la kutaka kusitishwa kwa mapigano Gaza mnamo Machi 25,2024
Baraza la Usalama la Umoja wa MataifaPicha: Andrew Kelly/REUTERS

Akilihutubia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa baada ya kura hiyo, Balozi wa Urusi Vasily Nebenzya amesema kuwa matumizi ya jana ya kura ya turufu ya ujumbe wa Marekani lilikuwa jaribio lisilo na matumaini la kusimamisha historia isiyoweza kuepukika.

Soma pia: Baraza la Usalama la UN halijaafikiana juu ya Palestina

Nebenzya pia amesema kuwa Marekani itajiondoa mara moja kwenye orodha ya mataifa yanayopenda amani na yanayoheshimika kwa madai ya kushirikiana kikamilifu na washirika wa Israel kwa vifo vya maelfu ya raia wa Palestina.

Marekani yasema haipingi kuweko kwa taifa la Palestina

Akielezea kuhusu kura hiyo ya turufu, mjumbe wa Marekani katika Baraza hilo Robert A.Wood, alisema kuwa Marekani inaendelea kuunga mkono kikamilifu suluhisho la mataifa mawili na kwamba kura hiyo haioneshi upinzani wake kwa taifa la Palestinalakini badala yake ni kuthibitisha kuwa litatokana na mazungumzo ya moja kwa moja kati yake na Israel.

Uingereza inasema lengo kwasasa ni kusitishwa kwa muda kwa vita Gaza na kuwaokoa mateka

Balozi wa Uingereza Barbara Woodward alielezea sababu ya kukosa kwa nchi yake kushiriki kura hiyo.

Woodward amesema kuwa hawakushiriki kwasababu lazima waangazie kwanza kusitishwa kwa muda kwa vita ili kuwanusuru manusura na baadaye kuchukuwa hatua za kusitisha vita kabisa bila kurudi kwenye uharibifu, mapigano na vifo.

Mjumbe wa Palestina katika Umoja wa Mataifa Riyad Mansour akizungumza katika kikao cha dharura kuhusu vita katika Ukanda wa Gaza mjini New York, Marekani mnamo Oktoba 26, 2023
Mjumbe wa Palestina katika Umoja wa Mataifa Riyad Mansour Picha: John Angelillo/newscom/picture alliance

Balozi wa Uswisi Pascale Baeriswyl, ameliambia Baraza hilo kwamba nchi yake ilikosa kushiriki kura hiyo bila kuipinga na kwamba wanaamini huu sio wakati mwafaka wa kufanyika kwake kutokana na mzozo unaoendelea.

Algeria yaahidi kurejea na nguvu zaidi

Balozi wa Algeria, Amar Bendjama, ambaye nchi yake ndiyo iliyowasilishwa rasimu ya azimio hilo, amesema, watarejea kwa nguvu na sauti zaidi na kwamba wataungwa mkono na idadi kubwa ya wanachama wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.

Palestina yasema haki yake ya kujitawala haiwezi kucheleweshwa

Balozi wa Palestina Riyad Mansour aliwaambia wajumbe wa Baraza hilo la Usalama kwamba haki yao ya kujitawala  haiwezi kubatilishwa, haifungamani na muda uliopangwa na kwamba ni ya milele na yenye ukuu.

Mansour ameongeza kuwa haki hiyo haiwezi kucheleweshwa au kuahirishwa.

Israel yaipongeza Marekani kwa kutumia kura yake ya turufu

Balozi wa Israel Gilad Erdan alianza hotuba yake kwa kuishukuru Marekani na hasa Rais wakeJoe Biden kwa kusimama na ukweli na maadili kati kati ya unafiki na siasa.

Erdan ameongeza kuwa alielezea jinsi Mamlaka ya Palestina isivyokidhi hata vigezo vya kimsingi na kukosa mamlaka juu ya eneo lake pamoja na kwamba inaunga mkono ugaidi.

Soma pia: Marekani yapiga kura ya turufu juu ya uanachama wa Palestina

Kupitishwa kwa rasimu ya azimio, kunahitaji kuungwa mkono na angalau mataifa tisa wanachama na kusiwe na kura ya turufu kutoka kwa mwanachama yoyote wa kudumu kama vile China, Ufaransa, Urusi, Uingereza na  Marekani.