Marekani yakanusha kumkwepa Netanyahu
12 Septemba 2012Awali vyombo vya habari vya Israel viliripoti kwamba Obama amekataa kukutana na Netanyahu wakati atakapokwenda Marekani baadae mwezi huu kwa ajili ya mkutano mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa kigezo cha kubanwa na raitba yake ya kazi.
Kwa mujibu wa Ikulu ya Marekani ni kwamba katika mazungumzo ya simu baina ya viongozi hao wawili hakukuwa na ombi lolote la mkutano kama huo na hakukuwa na jambo la kukataliana lolote.
Badala yake imesema viongozi hao walijadiliana kuhusu Iran na mpango wake wa nyuklia na mada nyingi kuhusu suala la usalama. Mapema kwa upande wake Msemaji wa Baraza la Usalama la Marekani Tommy Vietor alisema viongozi hao wawili hawataweza kukutana mjini New York kwa sababu ratiba yao ya kuwepo katika mji huo imepangwa kwa siku tofauti.
Rais Obama atawasili New York jumatatu ya Septemba 24 na kuondoka siku inayofuata wakati Waziri Mkuu Netanyahu anatarajiwa kuwasili katika jiji hilo mwishoni mwa wiki hiyo yaani baada ya Obama kuondoka.
Lakini hata hivyo alisema Obama na Netanyahu wanaendelea kuwasiliana na kwamba Waziri Mkuu huyo anatarajiwa kukutana na maafisa waandamizi wa Marekani akiwemo Waziri Mambo ya Nje wa Marekani Hilary Clinton.
Afisa mmoja ambae amenukuliwa na gazeti moja nchini Israel pasipo kutajwa jina lake alisema Netanyau aliomba kukutana na Obama katika ikulu yaMarekani mjini Washngton lakini Ikulu ililikataaa ombi hilo kutokana na harataki za kampeni ya uchaguzi.
Waziri Mkuu wa Israel Benjamini Netanyahu hivi karibuni amekuwa na maneno makali dhidi ya Marekani, kutokana na kile ilichodai Marekani inasita kuweka mpaka kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran.
Kati duru nyingine Waziri wa Ulinzi Ehud Barak, amemkosoa Netanyahu kwa kauli yake dhidi ya mshirika wake huyo mkubwa, Marekani. Barak amesema pamoja na kuwepo kwa tofauti na umuhimu wa kulinda uhuru wa Israel kutekeleza majukumu yake, lazima kukumbukwa umuhimu wa uhusiano wake na Marekani. Kutoka na umuhimu huyo basi Barak amemuhimza Netanyahu kujitahidi kwa kadili awezavyo kutouathiri.
Mwandishi: Sudi Mnette DPA
Mhariri: Mohammed Khelef