Marekani yakamata wanne kuhusiana na mauaji ya rais wa Haiti
15 Februari 2023Maafisa wa wizara ya sheria wametangaza mashtaka ya njama ya utekaji au mauaji nje ya Marekani, iliyopelekea kifo, dhidi ya wakaazi wa Florida, Antonio Intriago, maarufu kama Tony, Arcangel Pretel Ortiz na Walter Veintemilla.
Mshukiwa wa nne, Fredric Bergmann, anatuhumiwa kula njama kusafirisha kimagendo, vizibao vya kijeshi kwa ajili ya askari wa zamani wa Colombia wanaodaiwa kutekeleza mauaji hayo.
Naibu mwanasheria mkuu wa Marekani anaehusika na usalama wa taifa Matthew Olsen ameyataja mauaji ya Moise kama janga la kibinadamu na mashambulizi dhidi ya misingi ya kidemokrasia, ambayo athari yake kwa Haiti na watu wake bado inaendelea kuhisiwa hadi hii leo.
Soma pia: Raia wa Haiti akamatwa akihusishwa na mauaji ya Rais Moise
Wachunguzi wanadai wapangaji wa njama hiyo walikuwa na matumaini ya kuvuna kandarasi nono chini ya utawala mpya mara baada ya kumuondoa Moise.
Kwa mujibu wa wizara ya sheria, Intriago ndiye mmiliki wa kampuni ya ulinzi ya CTU yenye makao yake mjini Florida, ambayo inadaiwa kusaidia kuwaajiri wauaji. Ortiz pia ni mwakilishi mkuu wa kampuni hiyo.
Veintemilla, wakati huo, anatuhumiwa kufadhili operesheni hiyo kupitia kampuni yake ya Worldwide Capital Lending Group, ambayo inadaiwa kutoa mkopo wa dola 175,000 kwa CTU, na kutuma fedha kwa ajili ya ununuzi wa silaha.
"Mwishoni mwa Aprili 2021 Veintemilla na kampuni yake Worldwide (Capital Lending Group) walikubali kufadhili mapinduzi ya kijeshi," alisema Markenzy Lapointe, mwanasheria mkuu wa wilaya ya Kusini ya Florida.
Soma pia: Rais wa Haiti auwawa kinyama nyumbani kwake
"Veintemilla alitaraji kupata manufaa makubwa ya kifedha kupitia kampuni ya Worldwide endapo Moise angebadilishwa kama rais."
Mnamo Julai 2021, watu wenye silaha waliodai kuwa maafisa wa Mamlaka ya Kupambana na Dawa za Kulevya nchini Marekani (DEA) waliingia nyumbani kwa Moise katika mji mkuu wa Haiti wa Port-au-Prince na kumpiga risasi 12.
Mke wa marehemu rais huyo pia alijeruhiwa katika shambulio hilo.
Ombwe la mamlaka lililosababishwa na mauaji ya Moise limeruhusu magenge nchini Haiti kupata nguvu zaidi na kudhibiti maeneo zaidi, ambapo wataalam wanakadiria kuwa magenge hayo ya uhalifu yanadhibiti asilimia 60 ya mji mkuu Port-au-Prince.
Ongezeko katika visa vya utekaji, ubakaji na mauaji lilimlazimu kaimu waziri mkuu Ariel Henry kuomba majeshi ya kigeni, lakini ombi hilo la mwezi Oktoba halijazingatiwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, ambalo limechagua njia ya kutekeleza vikwazo mpaka sasa.
Watetezi wa haki za binadamu pia wanahoji uhalali wa Henry na kumlaumu kwa machafuko ya kisiasa baada ya kuahirisha kwa muda usiojulikana, uchaguzi wa rais na bunge uliopangwa awali kufanyika 2021.
Chanzo: Mashirika