Marekani yaiwekea Venezuela vikwazo vipya vya kiuchumi
29 Januari 2019Vikwazo hivyo vikali vilivyotangazwa siku ya Jumatatu na utawala wa rais Donald Trump vimeelekezwa haswa kwa kampuni ya mafuta ya petroli inayomilikiwa na serikali ya Venezuela PDVSA katika hatua inayolenga pia kuibana nchi hiyo mwanachama wa OPEC katika mauzo yake ya nje ya mafuta ambayo bado hayajasafishwa kwenda Marekani na wakati huohuo kumshinikiza rais Nicolas Maduro ajiuzulu kutoka madarakani.
Marekani sasa itazizuia mali za kampuni ya Venezuela PDVSA, zilizomo nchini mwake ambazo ndio chanzo kikubwa cha mapato ya Venezuela.
Rais Nicolas Maduro, katika hotuba yake kwa taifa, ameilaumu Marekani kwa kujaribu kuitwaa kwa mabavu kampuni tanzu ya Citgo ya usafishaji wa mafuta iliyoko nchini Marekani ambayo ni mali ya Venezuela inayosimamia pia vituo vya gesi vya nchini humo kwa niaba ya kampuni mama ya PDVSA, Maduro amesema Venezuela itachukua hatua za kisheria kuijibu Marekani.
Katika ishara ya kwanza ya kulipiza kisasi, vyanzo kadhaa vililiambia shirika la habari la Reuters kwamba PDVSA tayari imewaamuru wateja wanaosubiri kupakia mafuta ambayo hayajasafishwa kutoka Venezuela kwa ajili ya kupelekwa Marekani walipie huduma hiyo kabla ya kupokea mafuta la sivyo idhini haitatolewa ya kuzijaza meli au magari na pia meli hazitaruhusiwa kuondoka kutoka kwenye bandari ya Venezuela kabla ya malipo ya mafuta kufanyika.
Mshauri wa usalama wa taifa nchini Marekani John Bolton amesema vikwazo hivyo vitaitumbukiza Venezuela kwenye hasara ya dola bilioni 11 kufikia mwaka ujao na kwamba vitaizuia pia kampuni ya mafuta ya serikali ya Venezuela ya PDVSA kutumia mali zake zenye thamani ya dola bilioni 7.
Bolton ameeleza kwamba ingawa jeshi la Venezuela halijaonyesha ishara yoyote ya kumtelekeza Maduro lakini ana uhakika jeshi hilo linatambua hali tete ya uchumi na kwamba hatimae jeshi litafikia uamuzi wa kuiunga mkono na kuisadia serikali ya itakayoundwa na bunge la kitaifa.
Nchi kadhaa duniani kote zimemtambua kiongozi wa upinzani Juan Guaido, spika wa bunge la taifa la Venezuela, kama rais wa mpito wa haki, na Marekani imeapa kufanya kila jitihada kuutia njaa utawala wa Maduro kwa kuzuia mapato ya mauzo ya mafuta baada ya Maduro kuapishwa ili kuhudumu muhula mwingine mnamo Januari 10 baada ya kufanyika uchaguzi ambao unapingwa vikali.
Maduro naye ameapa kuendeleaa kutawala huku akiungwa mkono na Urusi na China, ambazo zinaipa fedha serikali yake na pia hivi majuzi zilipinga jitihada katika Umoja wa Mataifa za kutaka kupitisha hoja ya kutoitambua serikali ya Maduro.
Mwandishi: Zainab Aziz/RTRE/AFPE
Mhariri: Grace Patricia Kabogo