1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yaiwekea Urusi vikwazo vipya

17 Julai 2014

Marekani imeiwekea Urusi vikwazo vipya vinavyolenga uchumi wake kuhusiana na mzozo wa Ukraine.Urusi imeonya kuwa vikwazo hivyo vitaathiri uhusiano kati ya nchi hizo mbili na kuziathiri pia kampuni za Marekani

https://p.dw.com/p/1CeMW
Picha: picture-alliance/dpa

Umoja wa Ulaya na Marekani zimekuwa zikiitishia Urusi kuwa itawekewa vikwazo zaidi vitakavyouathiri uchumi wake ikiwa haitachukua hatua madhubuti kuhakikisha inaupunguza mzozo unaoendelea mashariki mwa Ukraine.

Licha ya Umoja wa Ulaya kuonekana kujikokota katika kuiwekea Urusi vikwazo,Rais wa Marekani Barrack Obama hapo jana alitangaza vikwazo vipya vinavyozilenga kampuni kubwa za Urusi katika sekta za fedha, kijeshi, nishati na watu binafsi wenye ushawishi.

Urusi yaonya vikwazo vipya vitakuwa na madhara

Putin ameonya kuwa vikwazo hivyo vipya vitakuwa na madhara makubwa na kuziathiri pia kampuni za Marekani zilizowekeza nchini mwake mbali na kuuzorotesha zaidi uhusiano kati ya nchi hizo mbili.

Rais wa Urusi Vladimir Putin
Rais wa Urusi Vladimir PutinPicha: Mikhail Klimentyev/AFP/Getty Images

Vikwazo hivyo vitaziathiri taasisi mbili za kifedha za Urusi ambazo sasa zitazuiwa kuendesha shughuli katika masoko ya fedha ya Marekani,kampuni mbili za nishati OA Novatek na Rosneft kampuni nane za kutengeza silaha na pia watu wanne wenye ushawishi serikalini.

Mkurugenzi mkuu wa benki ya Urusi VTB iliyowekewa vikwazo amesema vikwazo hivyo vipya sio sahihi na kuonya kuwa vitakuwa na madhara makubwa kwa mfumo mzima wa kifedha duniani huku naibu waziri mkuu wa Urusi Dmitry Rogozin akisema hatua hiyo ya Marekani si halali na ni njama ya uonevu inayonuia kuondoa ushindani kwenye soko la dunia.

Umoja wa Ulaya pia kuiwekea Urusi vikwazo

Wakati huo huo viongozi wa nchi za umoja wa Ulaya waliokuwa wakikutana mjini Brussels jana walisema pia nao wanajiandaa kutangaza vikwazo vipya dhidi ya Urusi baada ya kushauriana kwa kina na Marekani.

Viongozi wa nchi za Umoja wa Ulaya mjini Brussels
Viongozi wa nchi za Umoja wa Ulaya mjini BrusselsPicha: Thierry Charlier/AFP/Getty Images

Inatarajiwa kuwa Umoja wa Ulaya unatafakari kusitisha kuifadhili miradi ya maendeleo Urusi na vile vile kuzilenga kampuni ambazo zinaonekana kuuhujumu uhuru wa Ukraine.

Nchi kadhaa za umoja wa Ulaya zimekuwa zikisita kuiwekea Urusi vikwazo zaidi kutokana na hofu kwa kufanya hivyo itaathiri maslahi yao ya kibiashara na kuuathiri uchumi wao wenyewe.

Eneo la mashariki mwa Ukraine limekumbwa na ghasia ambazo zimesababisha vifo vya zaidi ya watu 600 na juhudi za kutafuta amani kufikia sasa hazijaweza kusitisha uasi katika eneo hilo.

Mwandishi:Caro Robi/Afp/Ap/Reuters

Mhariri: Daniel Gakuba