1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yaiwekea Tanzania vikwazo vya usafiri

1 Februari 2020

Rais wa Marekani Donald Trump ametangaza vikwazo vya utoaji viza kwa raia wa nchi sita ikiwemo Tanzania, kwa kuongeza kwenye orodha ya mataifa ambayo tayari yalilengwa katika mpango wake utata wa marufuku ya kusafiri

https://p.dw.com/p/3X7Kz
Tansania Daressalam Paul Makonda
Picha: DW/S. Khamis

Hatua hizo mpya pia zinazilenga Nigeria, Myanmar, Eritrea, Sudan na Kyrgyzstan. Maafisa wa serikali wamesema hatua ya Rais Trump ni matokeo ya uchunguzi mpana na wa kimfumo ambao ulifanywa na Wizara ya Usalama wa Ndani pamoja na ushirikiano na mashirika mengine ya serikali.

Marekani imesema uamuzi huo unatokana na nchi hizo kutotaka au kushindwa kuheshimu aina fulani ya usimamizi wa utambulisho wa kimsingi, kubadilishana taarifa na vigezo vya uchunguzi wa usalama wa taifa na usalama wa raia ambavyo vilianzishwa na wizara hiyo mwaka wa 2017. Aidha Wizara ya Mambo ya Nchi za Kigeni ya Marekani imempiga marufuku Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda kuingia Marekani. Taarifa ya wizara hiyo imesema Makonda anatuhumiwa kwa kuwalenga watu waliotengwa katika jamii wakiwemo mashoga, kuukandamiza upinzani pamoja na uhuru wa kujieleza.