1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yaitaka Uchina kuishinikiza Korea Kaskazini iweke wazi mpango wake wa nyuklia

26 Februari 2008

Waziri wa mambo ya nchi za nje nchini Marekani Condoleeza Rice amesema anatarajia China itasaidia katika kuishinikiza Korea

https://p.dw.com/p/DDMx

Waziri wa mambo ya nchi za nje nchini Marekani Condoleeza Rice amesema anatarajia China itasaidia katika kuishinikiza Korea Kaskazini iweke wazi mipango yake ya kutenegeneza zana hatari za Nyuklia.

Wakati huo huo Rice ambaye yumo mjini Beijing kwa ziara ya kikazi alikutana na waziri mwenzake wa mambo ya nje huko China Yang Jiechi na kiujadiliana naye kuhusu swala la zana za Nyuklia nchini Iran.

Juhudi za kujadili maswala ya nyuklia nchini Iran kati ya mawaziri wawili wa nchi za nje nchini Marekani na China waliokutana mjini Beijing, Condoleeza Rice na Yang Jiechi ziligonga mwamba walipotofautiana kuhusu jinsi ya kushughulikia swala hilo.

Baada ya mazungumzo hayo Rice aliambia vyombo vya habari kwamba baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linaendelea kutafuta azimio litakaloishawishi Iran iwache kuenda kinyume na jamii ya kimataifa.

Marekani ndio nchi iliyosimama kidete na kutaka jamii ya kimataifa iiwekee Iran vikwazo kutokana na mpango wake wa nyuklia.

Hata hivyo China imekuwa ikitoa wito wa mazungumzo kama suluhu katika swala hilo ambalo Marekani na nchi nyinginezo zinailazimisha Iran isalimishe madini aina ya uraniam ambayo zinahofia huenda yakatumiwa kutengenezea Nyuklia.

Waziri Yang amesema China ingali inaamini kwamba njia bora ya kutumika ni mazungumzo na kwamba matokeo ya swala hilo lazima yatokane na utatuzi wa amani.

Msemaji wa wizara ya mambo ya nchi za nje huko Marekani amesema nchi hiyo pamoja na nchi nyinginezo zinazoshinikiza vikwazo dhidi ya Tehran zinalitaka baraza la usalama la Umoja wa Mataifa lenye wanachama 15 kupata azimio haraka iwezekanavyo.

Iran imesisitiza kwamba mpango wake wa nyuklia unaendelea kwasababu za nishati inayotumika na raia wake.

Kwa upande mwengine Rice amesema anatarajia China isaidie katika harakati za kuishawishi Korea Kaskazini itangaze wazi mipango yake ya nyuklia huku akitumai kwamba harakati hizo zinatapata mwamko mpya iwapo China itaziunga mkono.

Alipokutana na waziri wa nchi za nje wa China Rice alisema anaendelea kungojea Korea Kaskazini itangaze wazi mpango wake wa nyuklia kama ilivyoahidi mwaka jana.

Yang amesema China imekuwa katika mazungumzo na Korea Kaskazini na kwamba anatumai awamu ya pili ya magumzo hayo itafaulu katika njia zisizokuwa na upendeleo wowote. China imekuwa ikisaidia kuinua tena uchumi wa Korea Kaskazini ambayo ni marafiki wa tangu jadi.

Wakati huo huo wizara ya nchi za nje nchini China imesema nchi hiyo na Marekani zimekubaliana kuanzisha tena mazungumzo kuhusu haki za kibinaadamu.

Msemaji wa wizara hiyo amesema makubaliano yaliafikiwa baada ya mazungumzo kati ya mawaziri wa nchi ya nje Yang Jiechi na Condoleezza Rice.

Marekani na China zilianzisha mazungumzo hayo mwanzoni mwa mwaka wa 1989 wakati wa mauaji ya kikatili ya Tiananmen yaliyoshuhudia vikosi vya China vikikabili vikali maandamano ya kupigania demokrasia na kusababisha vifo vya maelfu ya watu.

Hata hivyo mazungumzo hayo yalihairishwa kutoka mwaka wa 2004 baada ya Marekani kuwasilisha azimia kwa Umoja wa Mataifa wakiishutumu rekodi mbaya ya haki za kibinaadamu iliyowekwa serikali hiyo ya kikumunisti.

Rice yumo mjini Beijing kwa ziara ya kutembelea nchi tatu za barani Asia anayonuia kuitumia kuzishawishi nchi hizo ziungane kuunga mkono shinikizo dhidi ya Korea Kaskazini ili iheshimu makubaliano ya kusalimisha zana za nyuklia yaliyoafikiwa mwaka jana.

Amewasili mjini Beijing leo asubuhi kutoka Seoul na anatajajiwa kuelekea japan hapo kesho.