Marekani yaishtumu Iran kwa kukaidi azimio la UN
14 Mei 2020Ujumbe wa Marekani katika Umoja wa Mataifa ulitoa madai hayo katika mkutano usiokuwa rasmi wa wataalamu kutoka kamati ya baraza la usalama inayofuatilia utekelezaji wa azimio hilo.
Mzozo kati ya Iran na Marekani umeongezeka tangu utawala wa Trump kujiondoa katika mkataba wa nyuklia kati ya Iran na mataifa mengine sita yenye ushawishi mkubwa zaidi duniani mwaka 2018 na kuweka tena vikwazo vikali dhidi ya taifa hilo. Mwaka mmoja uliopita, Marekani ilituma maelefu zaidi ya wanajeshi wake na ndege za mashambulizi ya masafa marefu katika eneo la Mashariki ya Kati kujibu kile ilichokitaja kuwa tishio linaloongezeka la mashambulizi ya Iran dhidi ya maslahi yake katika eneo hilo.
Lengo la mkutano uliotishwa na Marekani
Mkutano huo ulioitishwa na Marekani hapo jana ulionekana kuwa hatua nyingine katika kampeini ya kuzidisha shinikizo kwa Iran kukoma kuingilia katika masuala ya eneo hilo na kukatiza kile ambacho Trump na Israeli wanaamini ni juhudi zake katika silaha za nyuklia madai yaliokanushwa na Iran.
Kikao hicho kiliandaliwa baada ya waziri wa mambo ya nje wa Marekani Mike Pompeo kufanya mazungumzo na waziri mkuu wa Israeli Benjamin Netanyahu wakati wa ziara ya ghafla ya siku moja na baada ya kuzungumza kwa njia ya simu na waziri wa mambo ya nje wa Estonia Urmas Reinslau ambaye nchi yake inashikilia urais wa baraza la usalama mwezi huu. Msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni Morgan Ortagus, amesema kuwa wawili hao walizungumza kuhusu ''juhudi za pamoja'' katika baraza hilo ''zinazolenga kuzuia mizozo na kuimarisha amani kote ulimwenguni.''
Taarifa kutoka ujumbe wa Marekani imesema kuwa taifa hilo liliibua suala hilo la urushaji wa setilaiti uliofanywa na jeshi la mapinduzi la Iran Aprili 22 katika mkutano huo wa Jumatano. Taarifa hiyo ililitaja jeshi hilo la mapinduzi kuwa ''shirika la kigaidi'' na kusema kuwa jukumu lake la uongozi katika mpango wa anga wa Iran linahitimisha madai ya Iran yasiokuwa na msingi kwamba mpango wake wa anga ni wa kiraia na kwamba hio sio hali sahihi.