1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yaisaidia Syria kuunda kikosi kipya cha jeshi

15 Januari 2018

Muungano wa kijeshi unaoongozwa na Marekani unashirikiana na wapiganaji wa Syria katika kuweka kikosi kipya cha askari 3,000, hatua iliyoipandisha hasira ya Uturuki.

https://p.dw.com/p/2qqx0
Irak YPG-Kämpfer

Hasira ya Uturuki ni kutokana na msaada wa Marekani kwa wanajeshi wa Kikurdi nchini Syria.

Afisa mmoja mwandamizi wa Uturuki ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa mafunzo ya Marekani yanayotolewa kwa kikosi cha ulinzi wa mpakani ndiyo sababu iliyofanya balozi mdogo wa Marekani kuitwa mjini Ankara Jumatano wiki iliypita.

Kikosi hicho cha jeshi ambalo kikundi cha mwanzo kinapewa mafunzo, kitawekwa kwenye mipaka ya eneo linalodhibitiwa na Wanajeshi wa Kidemokrasia wa Syria – SDF ambao ni muungano wa wapiganaji katika eneo la kaskazini na mashariki mwa Syria unaodhibitiwa na kundi la Kikurdi la YPG.

Naibu Waziri Mkuu wa Uturuki Bekir Bozdag amesema leo kuwa Marekani inacheza na moto kwa kuunda kikosi hicho.

Msaada wa Marekani kwa jeshi la SDF umeweka shinikizo

Jeshi hilo litawekwa kwenye mpaka Syria na Uturuki katika upande wa kaskazini, mpaka wa Iraq katika upande wa kusini mashariki, na kwenye Bonde la Mto Euphrates, ambao unatumiwa kama mstari unaotenganisha wanajeshi wa SDF wanaoungwa mkono na Marekani na wanajeshi wa serikali ya Syria wanapoungwa mkono na Iran na Urusi. Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Urusi Sergei Lavrov anasema kuundwa kwa kikosi hicho cha ulinzi wa mpakani huenda kukasababisha Syria kugawanywa katika maeneo.

Russland Sergei Lawrow bei seiner Pressekonferenz
Waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergei LavrovPicha: Getty Images/AFP/Y. Kadobnov

"Hatuoni juhudi za kusaidia kuutatua mozo huu haraka iwezekanavyo, bali tunaona juhudi za kuwasaidia wale wanaotaka kuchukua hatua za vitendo ili kubadilisha utawala katika Jamhuri ya Kiarabu ya Syria," alisema Lavrov.

Msaada wa Marekani kwa jeshi la SDF umeweka shinikizo kubwa kwa mahusiano yake na mshirika wa Jumuiya ya NATO Uturuki, ambayo inaliona kundi la YPG kuwa tawi la Chama cha Wafanyakazi cha PKK – kundi ambalo limeendesha uasi wa miongo mitau nchini Uturuki.

Makundi makuu ya Kikurdi nchini Syria yameibuka kuwa mojawapo ya washindi wachache wa vita vya Syria, na yanaweka jitihada za kuuimarisha udhibiti wao katika maeneo makubwa yaliyoyakamata kaskazini mwa Syria.

Marekani ina karibu wanajeshi 2,000 nchini Syria

Marekani inapinga mipango hiyo ya kujitawala, hata wakati ikiliunga mkono jeshi la SDF, ambalo ni mshirika mkubwa wa muungano wa kijeshi unaoongozwa na Marekani kwa ajili ya mapambano dhidi ya IS nchini Syria.

Syrien Kämpferinnen des SDF in Raqa
Wapiganaji wa kike wa SDFPicha: Getty Images/AFP/B. Kilic

Muungano huo umesema jeshi hilo la ulinzi wa mpakani litaendesha operesheni zake chini ya kamandi ya SDF na karibu askari 230 wanapewa mafunzo kwa sasa.

Marekani ina karibu wanajeshi 2,000 nchini Syria wanaopambana na kundi linalojiita Dola la Kiislamu – IS, na imesema imejiandaa kubakia nchini humo hadi pale itakapokuwa na uhakika kuwa IS imeanganizwa, kuwa juhudi za kurejesha utulivu zinaweza kudumishwa na kuna mafanikio ya kutosha katika mazungumzo ya Amani yanayosimamiwa na Umoja wa Mataifa kuhusu kuumaliza mgogoro huo.

Mwandishi: Bruce Amani/Reuters

Mhariri: Yusuf Saumu