Mkutano wa hali ya hewa.
28 Aprili 2009Baada ya sera ya miaka mingi ya kukwamisha juhudi, Marekani sasa inakusudia kushiriki katika harakati zinazoendeshwa duniani kote katika kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa.
Serikali ya Ujerumani imetiwa moyo na mtazamo huo mpya wa Marekani.
Mtazamo huo mpya umesisitizwa katika hotuba ya waziri wa mambo ya nje wa Marekani bibi Hillary Clinton kwenye kongamano juu ya nishati mjini Washington.
Hizo zilikuwa habari za kufurahisha kwa waziri wa mazingira wa Ujerumani Siegmar Gabriel.
Waziri Gabriel amesema viongozi wa siasa nchini Marekani sasa wanajizatiti katika ulinzi wa hali ya hewa. Waziri huyo ameeleza kuwa hayo hayakuonekana katika minne iliyopita.
Waziri Gabriel amesema utawala wa rais Obama umeamua kuwa na msimamo tofauti na ule wa utawala wa rais Bush juu ya suala la ulinzi wa mazingira.
Waziri wa Ujerumani amesema mtazamo mpya wa Marekani juu ya ulinzi wa mazingira siyo kauli tupu.
Msimamo huo ulisisitizwa na waziri wa mambo ya nje wa Marekani Hillary Clinton kwenye kongamalo juu ya nishati mjini Washington.
Bibi Clinton aliwaambia wajumbe kwamba mabadiliko ya hali ya hewa ni hatari ya kweli kwa dunia na lazima hatari hiyo ikabiliwe haraka. Amesema rais Obama na timu yake yote wapo tayari kuikabili changamoto hiyo.
Bibi Clinton ameeleza wazi kuwa Marekani haitajiweka kando tena.Amesema rais Obama na yeye mwenyewe wanaliweka suala la ulinzi wa hali ya hewa kwenye kitovu cha sera za nje za Marekani.
Mwandishi/Mtullya
Mhariri/Abdul-Rahman