Marekani yaathirika zaidi na virusi vya corona
3 Julai 2020Wakati Ulaya inaonekana kusogea katika ukurasa mpya katika mzozo huu mkubwa wa kiafya katika historia ya dunia, wasafiri wanaowasili nchini Uingereza kutoka Ujerumani, Ufaransa, Uhispania na Italia hawatalazimika kujitengwa kuanzia Julai 10.
Ugonjwa wa COVID-19 ukigusa karibu kila nchi hapa duniani, ugonjwa huo unaosababishwa na virusi , umefikia watu karibu milioni 10.7 na kusababisha vifo vya watu 516,000 duniani kote, na kuathirika uchumi ambao ulikuwa ukikua kwa kiasi kikubwa na kusababisha maisha ya jamii kusimama kabisa.
Wakati eneo kubwa la dunia likirejea katika hali ya kawaida , Marekani imefikia kesi zaidi ya 50,000 za maambukizi mapya jana kwa mara ya pili katika siku mbili, ikionesha hali mbaya katika sherehe zijazo za uhuru wa nchi hiyo.
Kwa hivi sasa ikiwa ndio kitovu cha janga hili, nchi hiyo imerekodi karibu vifo 129,000 kutoka zaidi ya kesi milioni 2.7 za maambukizi. Inatarajiwa kufikia idadi ya kesi milioni 3 za maambukizi wiki ijayo.
Ulaya yaanza kufungua mipaka
Lakini wakati baadhi ya magavana wa majimbo ya Marekani wakiweka sasa karantini ya siku 14 kw wasafiri kutoka katika majimbo yaliyoathirika zaidi, Umoja wa ulaya umeanza kufungua mipaka yake. Wakaazi wa Marekani , Brazil pamoja na Urusi iliyoathirika zaidi na virusi hivyo bado wananyimwa ruhusa ya kuingia katika mataifa ya Ulaya.
Shirika la afya ulimwenguni WHO limeonya siku ya Jumatano kuwa janga hilo linaongezeka, kwa zaidi ya nusu ya maambukizi ya dunia katika muda wa nusu ya mwaka katika mwezi Juni pekee. Na wiki iliyopita imeshuhudia viwango vya juu, wakati kesi zimefikia 160,000 katika kila siku moja ," Mkuu wa WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus alisema.
Idadi ya maambukizi imekuwa ikipanda katika mataifa ya Amerika ya kusini . Brazil ikiwa na uchumi mkubwa katika eneo hilo, ina karibu kesi milioni 1.5 zilizothibitishwa, ikiwa ni ya pili tu kutoka Marekani.
Idadi ya maambukizi nchini Ujerumani imeongezeka kwa watu 446 na kufikia watu 195,674, data kutoka taasisi ya Robert Koch ya magonjwa ya kuambukiza zimeonesha leo Ijumaa.
Korea kusini imeripoti maambukizi mapya 63 jana, wengi wao ni kutoka ndani ya nchi hiyo nje ya mji mkuu Seoul, na kusababisha kurejea kwa vizuwizi vikali vya kuzuwia kusogeleana wakati uwezekano wa wimbi la pili la ugonjwa huo likiwatia wasi wasi maafisa.