Marekani: Seneti lapinga sheria ya silaha
21 Juni 2016Hatua hiyo ya bunge, lenye wabunge wengi kutoka Republican, inaangaliwa kuwa na uhusiano na uhasama wa muda mrefu baina ya wafuasi wa chama hicho na Democrat, hasa katika wakati huu ambapo kinyang'anyiro kikali cha kampeni za urais kinaendelea.
Ukiwa umesalia mwezi mmoja tu kwa vyama vya Republican na Democrat kuwachagua rasmi wagombea wa urais, watunga sheria wanaelezwa kushindwa kufikia makubaliano juu ya suala hilo muhimu zaidi linaoikabili Marekani.
Pamoja na kwamba wanaonekana kutilia maanani umuhimu wa kuchukua hatua kufuatia tukio la mauaji ya kutisha zaidi katika historia ya Marekani yaliyotokea kwenye klabu ya usiku ya Orlando, na kusababisha vifo vya watu 49, wiki moja iliyopita, Republican na Democrat wamepiga kura ya kupinga mabadiliko manne ya sheria, mawili kutoka kila chama, ambayo yanalenga kuwepo kwa ukomo wa kununua silaha, ambazo ni pamoja na zile zinazohusishwa na matukio ya kigaidi.
Democrat inataka kuwekwa ukomo kwa wale walio kwenye orodha ya Shirika la Upelelezi la Marekani, FBI, kununua silaha, pamoja na kuboreshwa kwa uhakiki wa historia ya umiliki wa silaha kwa kuzingatia historia ya afya ya akili na matukio ya uhalifu kwa wale wanaohitaji kununua silaha katika maduka ya silaha ama kupitia mtandaoni.
Chama cha Republican kinapinga hatua hizo, huku kwa ujumla kikiunga mkono hatua zozote zinazolenga kuweka ukomo wa umiliki wa silaha, na wakisisitiza kuwa wanalindwa na Mabadiliko ya Pili ya katiba ya Marekani.
Wameunga mkono hatua ya kusubiri kwa masaa 72 kwa wale wanaotaka kununua silaha, ambao wamo katika orodha ya Shirika la Upelelezi la Marekani, FBI, ili kutoa nafasi kwa serikali kuomba kibali cha zuio la silaha kama kutakuwepo na haja ya kufanya hivyo. Aidha wanaunga mkono maboresho ya mfumo wa ukaguzi, ingawa Democrat wanapingana nao.
Seneta Chriss Murphy wa chama cha Democrat, jimbo la Connecticut, kwa upande wake amesema, hatua iliyofikiwa sasa nchini humo si ya kuendelea kufanya mazungumzo bila ya kuchukuliwa kwa hatua zozote.
Hatua kama hizo mara zote hulipambanisha bunge, ambapo huhitajika kura 60 kati ya 100, ili kuendelea kujadiliwa.
Bunge la Seneti liliwahi kupitisha hatua kama hizo baada ya tukio la mauaji yaliyotokea kwenye shule ya Connecticut, mwaka 2012 na San Bernardino mwaka jana, lakini hazikuwa na matokeo yoyote.
"Kila seneta anataka kuondolewa kwa uwezekano wa magaidi kumiliki silaha wanazotumia kwa mauaji ya raia wasio na hatia, lakini kuna namna unaweza kufanya mambo kwa usahihi ama kwa ubaya", alisema Seneta wa Republican wa Texas, John Corny.
Bunge la Marekani, lina wabunge 46 kutoka chama cha Democrat au wanaounga mkono chama hicho na 54 kutoka Republican.
Mwandishi: Lilian Mtono/AFP
Mhariri: Mohammed Khelef