Marekani na Urusi zaujadili mzozo wa Syria
18 Septemba 2017Tillerson na Lavrov wamekutana jana mjini New York, kabla ya kuanza kwa mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa. Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani, Heather Nauert amesema kuwa viongozi hao wamekubaliana kujiepusha na mapambano ya kijeshi nchini Syria, kupunguza ghasia na kuanzisha masharti ili mchakato wa Geneva uweze kusonga mbele.
Tillerson hakuzungumza na waandishi
Baada ya mkutano wa mawaziri hao, uliofanyika kwenye ubalozi wa Urusi katika Umoja wa Mataifa, Tillerson aliondoka bila ya kuzungumza chochote na waandishi habari, ambao awali walialikwa kuhudhuria mazungumzo hayo, lakini baadae walitakiwa kuondoka baada ya kuwasili kwa afisa wa Marekani.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Urusi, Maria Zakharova, amewaambia waandishi habari kwamba mkutano ulihusu ushirikiano katika mzozo wa Syria, masuala ya Mashariki ya Kati na makubaliano ya Minsk. Hata hivyo alipoulizwa namna mazungumzo hayo yalivyokwenda, alijibu kuwa hana taarifa kwa sababu hakuwepo ndani ya chumba cha mazungumzo.
Uhusiano kati ya Marekani na Urusi uko katika kile ambacho Tillerson amekiita wa ''kihistoria'' baada ya Vita Baridi wakati ambapo nchi hizo mbili zimekuwa zikilipiziana kisasi katika masuala ya kidiplomasia. Lakini Marekani inataka kufanya kazi na Urusi ili kusaidia kuutatua mzozo wa Syria, ambako nchi zote mbili zina vikosi vyake na wapinzani wakijaribu kuendesha shughuli zao kutokana na tofauti hizo walizonazo.
Rais wa Urusi, Vladmir Putin hatohudhuria mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa unaofanyika wiki hii, lakini Rais wa Marekani, Donald Trump anatarajiwa kutoa hotuba yake ya kwanza katika baraza hilo hapo kesho.
Urusi na Marekani zatupiana lawama
Hata hivyo, mazungumzo hayo kati ya Urusi na Marekani yamefanyika baada ya Urusi kushutumiwa kuvilenga vikosi vinavyoungwa mkono na Marekani katika mapambano dhidi ya kundi linalojiita Dola la Kiislamu, IS katika shambulizi la anga. Hayo yameelezwa jana na kamanda wa jeshi la Marekani.
Vikosi vinavyopigania demokrasia nchini Syria, SDF, vinavyojumuisha wapiganaji wa Kikurdi na Kiarabu na vinavyoungwa mkono na Marekani, vimesema kuwa wapiganaji wake walijeruhiwa katika shambulizi la ndege za kivita lililofanywa na Urusi mashariki mwa Mto Euphrates karibu na jimbo lenye utajiri wa mafuta la Deir al-Zor.
Msemaji wa jeshi la Urusi amekanusha madai hayo, ingawa jeshi la muungano limekiri kwamba Urusi ilikuwa ikifahamu kuwa eneo hilo lina wapiganaji wa SDF. Vikosi vya SDF na majeshi ya serikali ya Syria yanayoungwa mkono na Urusi yanaendesha operesheni zenye malengo sawa lakini yanayotofautiana, dhidi ya wapiganaji wa jihadi katika jimbo la Deir al-Zor, jimbo kubwa ambalo bado linadhibitiwa na IS.
Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFP, Reuters
Mhariri: Josephat Charo