Marekani na Urusi yabadilishana mawakala wa ujasusi
10 Julai 2010Moscow.
Urusi na Marekani zimetekeleza mabadilishano makubwa ya majasusi tangu kumalizika kwa vita baridi, yaliyofanyika katika uwanja wa ndege wa Vienna, nchini Austria. Ndege moja iliwaleta mawakala 10 wa Urusi walioachiwa kutoka Marekani baada ya kikao cha mahakama , ambapo walikiri kufanya upelelezi wa kijasusi. Ndege nyingine iliripotiwa kuwa na watu wanne ambao walihukumiwa kufanya ujasusi nchini Urusi, ambao wamepewa msamaha wa rais baada ya kutia saini taarifa kuwa wana hatia. Mmoja kati ya wale waliohusika katika ubadilishanaji huo, ni mtaalamu wa masuala ya kinuklia Igor Sutyagin ambaye alifungwa jela nchini Urusi mwaka 2004. Kaka yake Dmitry amesema kuwa Igor atawasili nyumbani hivi karibuni. Tukio lote hilo limekamilika haraka , hali inayoashiria kuwa Urusi na Marekani zote zina nia ya kuepusha athari katika uhusiano wao.